Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Januari 08, 2017

Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana

Isa 42: 1-4, 6-7;
Zab 29: 1-4, 9-10;
Acts 10: 34-38;
Mt 3: 13-17.

UBATIZO KAMA WA WATOTO WA MUNGU!

Sikukuu ya leo, inamalizia kipindi cha Noeli na kuanza kipindi cha Mwaka wa Kanisa. Ni sikukuu inayo onesha mpito wa Yesu kutoka katika utume wake uliofichika na kuanza utume wa hadharani. Ubatizo wa Yesu una dhihirisha ‘Umungu wa Yesu kwa wafuasi wote wa mwanzo na kwa wanafunzi wa yohane Mbatizaji.

Je, ni kwanini Yesu aliruhusu Yeye mwenyewe kubatizwa? Hakuhitaji ubatizo, wala kutubu kwani yeye hakuwa na dhambi. Siajabu Yohane Mbatizaji alishangazwa sana: “Yohane anasema ninapaswa ni batizwe nawe, nawe umekuja kwangu mimi.” Yesu alitaka kuonyesha umoja wake na wanadamu, kujihusisha mwenyewe moja kwa moja na wanadamu wadhambi ili awaokoe kutoka dhambini. Kilikuwa ni kitendo chake mwenyewe. Ubatizo wa Yesu unatabiri kifo chake mwenyewe, ufufuko na Ujio wa Roho Mtakatifu kama Yohane alivyoweka: “Yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na moto.”

Ubatizo wa Yesu ulikuwa ni wa lazima kwasababu kwake yeye ulikuwa ni muda wa maamuzi. Ulitoa ishara kwa Yesu kuanza utume wake. Yesu anachukua changamoto
ya Mungu kwa kufanya uamuzi wa kuanza utume wake ulimwenguni. Ubatizo wa Yesu kwake Yeye ulikuwa ni wakati wa utambulisho. Ulikuwa ni muda kwake yeye kujitambulisha mwenyewe pamoja na Mungu. Na Yesu anajua anafanya haya kwa ajili yetu sisi. Ubatizo wa Yesu ulikuwa ni wakati wa kuthibitishwa kwake. Yesu alikuwa tayari kuchukua utume wake na alipokea wakati huu wa thibitisho la Mungu: “Huyu ni mwanangu mpendwa.” Ubatizo wa Yesu kwake yeye ulikuwa ni wakati wa pekee. Mungu anatutaka sisi tumsikilize Mwanae. Sisi tujifunze kumsikiliza Yesu katika maandiko Matakatifu, licha ya sauti mbali mbali zilizopo Ulimwenguni, tujifunze kumsikiliza Yesu na kumchagua yeye pekee. Ujumbee anaotangaza nabii Isaya katika somo la kwanza kuhusu mtumishi wa Mungu, unatimilika ndani ya Kristo katika ukamilifu wote kama Injili inavyo mdhihirisha. Ndivyo anavyo lidhihirisha hilo mtume Petro katika somo la pili, kwamba Yesu ni mteule wa Mungu. Yeye anaponya madhaifu yote na kutufanya tuwe kuru kwa kututoa gizani na kutufanya watoto wa Mungu.

Yesu aliileta Habari Njema, ujumbe wa amani tofauti na ujumbe wa Yohane, Yesu yupo tayari sasa kuushinda ulimwengu kwa upendo."Ubatizo Mtakatifu ni msingi wa maisha yote ya Kikristo, mlango wa kuingilia uzima katika Roho, na mlango unaowezesha kuzipata sakramenti nyingine." (Katekisimu ya Kanisa Katoliki - 1213). Katika ubatizo wetu Mungu “anafungua mbingu” na anatutumia Roho wake Mtakatifu; mbingu iliyofungwa kwa dhambi ya Adamu na Eva sasa imefunguliwa. Katika ubatizo Roho Mtakatifu anachukua nafsi zetu, anazitakasa, na anazifanya kuwa makao yake yanayofaa.


Kwetu pia anasema katika ubatizo: “Huyu ni mwanangu mpendwa.” Ubatizo unatufanya sisi kuwa watoto wakweli wa Mungu. Kama Yesu sisi pia tunapaswa kuongozwa na Roho na kuwa tayari kutekeleza utume uliokabidhiwa kwetu. Maisha yetu yote yanapaswa yawe “Habari Njema” kwa wengine, kwa kuwasaidia na kutenda mema, hususani kwa
wahitaji.

Sala: Bwana, Nisaidie kutambua kuwa Mimi ni mwanao. Yesu nakuamini wewe. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni