Jumatatu, Novemba 15, 2021
Jumatatu, Novemba 15, 2021.
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa
1 Mak 1: 10-15, 41-43, 54-57, 62-64;
Zab 118: 53, 61,134, 150, 155, 158;
Lk 18: 35-43.
FUNGUA MACHO YA MOYO WANGU, NINATAKA KUKUONA WEWE
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo linaongozwa na maneno ya mzaburi katika wimbo wa katikati-Ee Bwana unijalie uhai nami nitazitii kanuni zako. Maneno haya siku ya leo yanatuchimbulia chimbuko la somo letu la kwanza leo.
Hapa tunakutana na simulizi ya mfalme aitwaye Antiochus Epiphanes aliyewaletea madhara makubwa sana Waisraeli; alitaka kuangamiza Imani na tamaduni za Kiisraeli na kufanya Mungu asiheshimiwe tena. Akaweka amri ati atakayekutwa amebeba kitabu cha maandiko matakatifu auawe. Akawaambia watu wageukie kwenye uabudu wa sanamu na kutolea uvumba masanamu na baadhi ya Wayahudi hasa wale vijana vijana walikubaliana na hili wakaona sawa wakasema tuachane na hivi visheria vyetu vya Kiyahudi, vinatubana sana, tunashindwa kuoana hata na watu wa mataifa, tunashindwa kula raha kama watu wa mataifa. Hivyo, walianza kukumbatia haya mambo ya kimataifa na kuiacha Imani yao.
Kitu hiki kiliwauzi baadhi ya Wayahudi na hivyo kulitokea kikundi cha Wamakabayo kilichopingana na huyu mfalme na wafuasi wake wote waliokuwa na lengo la kuiteketeza dini ya Kiyahudi (Judaism). Hivyo, wimbo wa katikati unaakisi dhamira ya hiki kikundi cha watu-unijalie uhai ee Bwana nami nitalisifu jina lako.
Hii ndio nia ya hawa Wamakabayo ambao kitabu chao tutakisikia kwa siku kadhaa kadhaa. Hawa ni watetezi wa dini ya Kiyahudi. Wanasema unijalie uhai ee Bwana nami nitakuonesha jinsi nitakavyolifanya jina lako lisifiwe, sitaliacha lidhihakiwe na hawa watu.
Katika somo la injili, tunakutana na kipofu anayelia Bwana nionee huruma-nionee huruma Bwana nipate kuona. Huyu naye ukimchunguza utaona kwamba mawazo yake ni kwamba nijalie nipate kuona ee Bwana halafu nitakuonesha namna jinsi ninavyokupenda, nitawasimulia watu wote juu ya ukuu wako. Niponye tu na hapo utashuhudia mwenyewe.
Ndugu zangu, makundi yote mawili-Wamakabayo wa somo la kwanza na kipofu wa somo la injili walifanikiwa kwa kile walichoomba. Hawakushindwa ndugu yangu kutokana na kupania kwao kumtumikia Bwana.
Ndugu zangu, hapa nasi tunajifunza kitu. Sisi tunashida mbalimbali, twende kwa Bwana, mwambie ee Mungu niponye tu, nisaidie tu jamani, fanya kitu na watu wote watashuhudia-watashuhudia jinsi nitakavyokutangaza, yaani wekeza kwangu ee Bwana na nakwambia sitakuangusha, mwambie Bwana hivi ndugu yangu na nakwambia atakusikiliza tu.
Lakini siku zote uwe na lengo jema, sio kwa ajili ya kuwatesa wengine au kuwaonea wengine au utembee mbele uitwe bosi, bosi bosi au uitwe mkuu mkuu-lengo lisiwe hili. Lengo liwe ni kumfanya Mungu atukuzwe na si wewe uitwe mkuu, mkuuu, jembee, jembee!
Kingine ni kwamba huzunika popote uonapo jina la Mungu likidharaulika kama wale Wayahudi tuliosikia katika somo la kwanza. Yaani ilifikia mahali ikawa kushika hata yale maandiko yao matakatifu ikawa ni adhabu. Jina la Mungu wao likawa linadhihakiwa lakini baadhi hawakuvumilia hili. Nawe ndugu yangu usikubali jina la Mungu lidhihakiwe. Ukipita ukikutana hata na rozari imetupwa inakanyagwa kanyagwa huko iokote, ukiona picha ya Yesu inakanyagwa huko iokote, ukiona Biblia ipo kwenye sehemu chafu iokote na usafishe hilo eneo, ukiona vitambaa vya altare ni vichafu na vimeshachakaa tayari kazana vingine vinunuliwe. Jina la Bwana lisidhihakiwe hata kidogo.
Maoni
Ingia utoe maoni