Jumapili, Novemba 14, 2021
TAFAKARI YA DOMINIKA YA 33 YA MWAKA B WA KANISA
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu Jumapili ya leo ambapo ni jumapili ya 33 ya mwaka B wa kanisa. Zaburi yetu ya wimbo katikati inatuambia Mungu unihifadhi mimi kwa maana nakukukimbilia. Bwana ndiye fungu la posho langu, yeye ndiye mwenye kuishika ahadi yetu milele nami nimemuweka Bwana wangu daima kwa kuwa, yumo kuumeni mwangu, sitaogopa.
Hii ni zaburi aliyoiimba Daudi akiwa kama mfalme amezungukwa na ma-body guards wengi. Lakini akawa bado na wasiwasi na kuona kwamba lazima nitafute ulinzi zaidi kwani huu hautoshi na ndivyo akaomba ulinzi toka kwa Mwenyezi Mungu.
Siku ya jumapili hii ya leo zaburi inatumika kumhimiza kila mmoja kutafuta ulinzi toka kwa Mwenyezi Mungu kwani mambo yana mwisho, hawa wakuu, wafalme, weenyewe, na watu maarufu yana mwisho.
Somo letu la kwanza na injili yetu inaelezea vizuri ujumbe huu. katika somo la kwanza, nabii Daniel anaeleza uwepo wa siku ya hukumu na hii itakuwa ni siku mbaya kwa wale walioishi kiholela holela tu. Ujumbe huu ilibidi awaeleze baadhi ya wana wa Israeli ambao kwa kipindi hiki kutokana na ukweli kwamba walikuwa wakiteswa na mfalme mpagani aliyeitwa Antiokus, wengi waliianza kuiacha dini yao, wakabadili hata majina yao ili wasitambulike kwamba ni Wayahudi ili wapatiwe ajira kwenye utawala wa Antiokus.
Mfalme huyu hakumwajiri Myahudi kwenye serekali yake-wale wanaoshika dini. Wengi waliogopa kuiungama dini yao hadharani na kugeukia miungu ile ya wagiriki ili wapate vyeo ndani ya ile serekali ya Antiokus.
Mwandishi anawaeleza acheni kuiacha dini yenu, msitafute kuajiriwa au vyeo mkaacha dini yenu. Siku inakuja ambapo dunia hii itafikia mwisho na wale waovu kuhukumiwa. Hata huyu Antiokus mnayemuungama ataanguka tu. Ishikeni dini yenu.
Maneno haya anatueleza na sisi pia-tujiullize ni wapi tumelegea kushika dini yetu? Wengi tunaona aibu, ukiambiwa uvae rozari unaona aibu, ukiambiwa usalishe unaona aibu ati utaonekana mshamba. Au kanisani unakaa mwisho uonekane mjanja-wanaokaa mbele ni wajinga-huku ni kuzembea. Ni kama padre aogope kuvaa nguo zake au sista akatae yale mavazi yake. Ataonekana kuwa kituko. Hapa ni kushindwa kumshuhudia Kristo kwa hadharani kabisa.
Tuzidishe imani yetu katika kumshuhudia Kristo.
Hata baadhi yetu tunabadili dini tuolewe, au tupate kazi au tunabadili jina tupate kuajiriwa. Huku ni kuishi kana kwamba mwisho wa mambo yote ni hapa duniani. Ni kushabikia shabikia tu watu.
Zaidi ni kutokuruhusu vitu kama uzuri au pesa zikufanye uwe na kiwewe kana kwamba utaishi milele. Mara nyingi ukikutana na wasichana wenye sura nzuri, wale weupe weupe unakuta hawajaolewa na wengi wanaishi maisha ovyo na majivuno mengi, wanaishi na mwanaume huyu, yule na ubabe mwingu. Ndugu yangu kuwa na msimamo. Uzuri ni kitu kidogo sana. Si mnajua kwamba inafikaga wakati unaishaga ee? Si ndio, sasa? Tuwe na msimamo jamani.
Au wale wavulana wenye pesa, au hawa wanamuziki hawa na wenye vipaji kama wachezaji, utakuta hawa watu wanaishi maisha yasiyoeleweka, jamani, unajiuliza, hawa watu ni miungu au? Wanajua kwamba kuna mwisho? Jamani, tusiweweseke hivyo. Lazima tubadilike.
Katika injili, Yesu anazungumzia juu ya ujio pia wa wakati wa mwisho. Anasema jua litatiwa giza na mwezi hautatoa mwanga wake. Jua na mwezi ni vitu muhimu sana kwa ulimwengu. Ndizo zinazoongoza majira mbalimbali ya hapa duniani. Ndizo zinazosaidia dunia ione mwanga na viumbe vya ulimwengu viishi kwa kupata hewa na maji. Lakini tunaelezwa kwamba haya yote yatakomeshwa. Ujumbe wa hapa ni kwamba hakuna kitakachodumu milele.
Jua na mwezi vinamaanisha pia watu maarufu na wakuu fulani hivi. Hawa watu maarufu, wasanii, matajiri, wasomi, wanasayansi watakuwa na mwisho kama inavyotokea kwa jua na mwezi. Hapana haja ya kumuungama hata mmoja au kumsujudia kama Mungu. Wao watakwenda tu.
Lakini ukweli ni kwamba nguvu zitakazofanya ulimwengu uanguke haimaanishi kwamba ni lazima zitoke kwa Mungu tu. Nyingine zitaanzia kwa wanadamu.
Kwa mfano, angalia jinsi pale wanadamu walivyotumia akili yao vibaya na kutengeneza silaha za nuclear ambazo hadi sasa wanazitumia kuangamiza ulimwengu. Kweli mwanadamu inambidi awe na hekima kwenye kutumia akili yake vyema, aonyeshe hekima ya kutosha.
Tabia za umbea na fitina ni vitu vingine vinavyoangamiza jamii yetu. Tayari zimekwisha leta giza ndani ya familia nyingi sana na kila upitapo kweli wamesababisha fujo. Ni vitu ambavyo papa Fransisko anasema vinaangusha bomu katikati ya watu na kujeruhi wengi na tayari wengi wamekwishanyongonyeshwa na mambo haya. Ni lazima kuyapinga kwa kisawaswa kabisa. Vinatuletea giza.
Kingine ni utumizi wa haya ma-gadgets na mtandao. Haya yanapoteza udugu wetu. Siku hizi watu hatujuliani hali tena, wale tuliokaribu. Unakuta mtu anamjulia hali kwanza mtu aliyemarekani na kuaachana na huyu aliyeko pembeni yake. Mwisho wa siku tunakua bila kujuana na majirani zetu, tunakazana kujenga urafiki na watu wasioonekana na wengine hata hawapo na kuwaaacha wale tunaowaona hapahapa machoni petu. Kweli ni kitu kingine kinachoimaliza dunia na jumuiya zetu.
Kingine ni ulaji mbovu-wa pombe na sukari. Hizi jamani kuna watu wengi wamekwenda kwa ajili haya. Angalia jinsi kisukari na kansa kilivyochukua wengi? Wakati mwingine ni kutokana na ulaji mbaya, watu bila kujali, tamaa tu. Wengi pia hata hawafuati masharti, ukimweleza mtu kwamba umefungiwa pombe, kweli atakasirika kweli, na wengine watakiuka hata masharti na kweli wanakwenda ee. Haya ni mambo kweli yanayoifanya dunia yetu iangamie.
Lakini zaidi siku ya leo ni kuendelea kubakia katika imani, kutambua kwamba maisha yetu yanamwisho, tushuke chini na kutumikiana. Hata kama ni cheo chako, hata kama ni akili yako, uzuri wako, pesa zako, umaskini wako usikubali ukuangushe. Tulia.
Maoni
Ingia utoe maoni