Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Novemba 13, 2021

Jumamosi, Novemba 13, 2021.
Juma la 32 la Mwaka

Hek 18: 14-16; 19: 6-9;
Zab 105: 2-3, 36-37, 42, 43;
Lk 18: 1-8.


KUVUMILIA UKIWA KATIKA SALA!

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na mwandishi wa kitabu cha Hekima ya Sulemani akiongea na watu wanaojiona kuwa ni wanyonge katika taifa jingine, yaaani Wayahudi wakiwa mjini Alexandria. Huko wanakejeliwa na wanaphilosophia kama akina Epicureans(wanao amini maisha ni hapa duniani tu, hivyo ponda raha iwezekanavyo, wala usijihusishe na maskini kwani watakuletea shida zao na hapo utashindwa kuponda raha).

Lakini mwandishi anawafundisha juu ya silaha wanayopaswa kutumia ili kukabiliana na hawa watu. Anawaambia waendelee kungangania hekima ya Mungu. Hii ndiyo iliyomwezesha Musa kufanya miujiza yote na kuwawezesha waisraeli kuvuka bahari ya shamu na kuwaokoa katika mapito yote. Hekima hiyo hiyo ndiyo iliyowaangamiza Wamisri kwa ile miujiza na walipokuwa katika bahari ya shamu. Sasa mwandishi anawaambia waitafute silaha hii nao wataweza kuishi, hata kupambana na kejeli za Epicureans.

Katika injili tunakuta na mwendelezo wa kitu kama hiki. Yesu anamfundisha silaha anayopaswa kuwa nayo yeyote aliye na Imani-na anayesumbuliwa na mapito ya kimaisha kama hawa Wayahudi walipokuwa huko Alexandria. Anawaambia kwamba wanapaswa kuwa na uvumilivu katika sala. Hii ndiyo hekima na silaha ya mnyonge, hii ndiyo itakayomwezesha kuvuka katika mapito yote.

Tunaalikwa kutumia silaha hizi kama Ayubu alivyotumia ile yake ya uvumilivu kupita mapito yake, kama Daudi alivyotumia Imani yake kupita mapito yake kumshinda Sauli na kama Abrahamu alivyotumia Imani yake kupita mapito yake hata kwenda nchi asiyoijua aliyotumwa na Mungu.

Sasa Yesu anatuambia katika injili kutafuta silaha zetu na kuzitumia katika kuvuka. Yesu anatuambia kwamba nasi tukitumia silaha ya uvumilivu, tutashinda, tutavuka na kuingia palipo pakavu kama wanawa Israeli walivyoweza kuvuka katika bahari ya shamu.

Hivi ndivyo Imani yetu inavyotudai ndugu zangu na ndizo silaha tunazopaswa kutumia. Ukizikataa silaha hizi, nakwambia itakuwa ni majanga tu katika maisha. Kwani maisha yana mapito mengi, kuna hali mbalimbali zinazojitokeza katika maisha. Unaweza kujiona unacheka sasa, lakini kunatokea kitu na kufuta furaha zote. Rafiki unayemtegemea au hata ndugu yako au hata mtoto anaweza kukutendea kitu usichotegemea. Kama huna silaha kama hizi katika maisha yako au Imani yako kwa kweli hutaweza kumudu uhalisia wa maisha.

Hata sala yenyewe ilivyo: unajikuta wewe umepanga mipango yako namna hii, unataka mambo yako yaende namna hii lakini Mungu anao mpango tofauti juu yako. Anamipango yake tayari. Hivyo, pasipokuwapo uvumilivu katika Imani, utajikuta kila siku unaishia katika kumlaumu Mungu. Hivyo ndugu zangu tujue silaha zetu ni zipi na tuzikimbilie.

Tuzikimbilie hasa tunapokutana na vitu vya ajabu katika Imani yetu. Unaposhangaa kuona kwamba mwenzako kakutendea kitu cha ajabu katika maisha yako. Yaani, unakuta mtu usiyemtegemea amekutendea kitu usichokitegemea kabisa. Sasa silaha hizi zitakuwezesha kupita hapa.kuna wakati utadhaniwa vibaya na kudharaulika ndio wakati wakutumia silaha kuhakikisha umebaki katika umoja na Mungu, kubaki katika hiyo hekima ya Mungu, kwani matukano au vigelegele vya watu juu yako havikufanyi wewe kuwa mbaya au kuwa Mtakatifu.

Maoni


Ingia utoe maoni