Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Novemba 10, 2021

Jumatano, Novemba 10, 2021.
Juma la 32 la Mwaka

Hek 6: 1-11;
Zab 82: 3-4, 6-7 (K) 8;
Lk 17: 11-19.


SHUKRANI!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na mwandishi wa kitabu cha Hekima akiwaambia wanaoitwa kuwa wakuu kati ya watu wamtambue Mungu kama mtoaji wa huo ukuu. Wasijione kana kwamba ni miungu, kana kwamba wao kwa kitendo cha kufanikiwa kidogo sasa wana uwezo wa kila kitu ndani ya hii dunia. Wasifikiri kwa kitendo chao cha kuheshimiwa na kusalimiwa na watu na kuitwa wazee na waheshimiwa, wasijione kwamba ati wao wamechukua nafasi ya Mungu.

Twaweza kusema wakumbuke kwamba siku kadhaa zilizopita walikuwa tu wanavaa kaptura kama wanafunzi wa primary, walikuwa maskini tu, hawakuwa wanakula hata chakula cha mchana-lakini sasa wamepata kacheo na kuanza kuitwa waheshimiwa na wanaanza kutaka kuchukua nafasi ya Mungu na kutaka na wao ati watawale na kuchukua nafasi ya Mungu. Ni vizuri kuangalia kama unaiba sifa za Mungu.

Injili ya leo inaendeleza maada hii kwa kutuonesha mfano wa watu waliofanya hivi. Hawa walikuwa ni wale wakoma tisa kutoka Uyahudi waliokataa kurudi kwa Yesu kutoa Shukrani zao. Hawa mwanzoni walikuwa watu maskini, wametengwa, hawana hata nguo-sasa wanapopona wanaenda sasa huko mtaani wanaanza kuruka, labda wataanza kuwatukana hata wenzao walio na ukoma, labda wataanza kuwapiga hata watu na kuanza kuwaonea, Yaani walishindwa nakusahau ile hali yao ya zamani, ule ugonjwa wao, ule unyonge wao na sasa wanajiona kuwa ni mabosi. Hata kwa Yesu hawafiki tena. Hawa ndio wakoma wetu. Lakini siku chache zilizopita walikuwa ni ombaomba huko lakini sasa Yesu kawaponya hawaonekani.

Labda na kwako ndugu iko hivi. Wewe yawezekana miaka kadhaa hapo ulikuwa huna chochote, nyumba huna na sasa umemwomba Mungu kakupa lakini umemsahau kwamba ndiye aliyekupa na sasa unaonea wenzako, ukipita barabarani na gari hujali, unatukana, majirani zako huwaoni kuwa kama kitu, nakwambia angalia vizuri ndugu yangu. Kumbuka ulikotoka. Usitese watu na mali za Mungu. Mungu hakukupa ili uwatese wenzako. Angalia utaweza kugeuka maskini baada ya masaa kadhaa.

Kingine tujue kwamba kukataa kutoa shukrani ni kushindana na Mungu. Unataka kuchukua nafasi yake, unataka uonekane kwamba mafanikio uliyoyapata ni ya kwako, kama mtu anayefanya kukopi kazi ya mtu, anayetumia kazi ya mtu bila kusema (kuaknowledge) na kujifanya ni yake-ndivyo hivyo ilivyo kwa asiyetoa shukrani. Ni kushinda na Mungu na anayeshindana na Mungu ni shetani-ndio kazi yake. Adhabu ya anayefanya kunakili kazi ya mtu bila kusema nakujifanya yake ni kunyanganywa ile hadhi aliyokuwa amejinyakulia kwa kitendo chake cha kutumia hiyo kazi ya mtu mwingine.

Hata sasa tutambue kwamba kama tutakosa shukrani kwa Mungu, adhabu yake ni kunyanganywa ile hadhi uliyokuwa nayo, hadhi ya kuwa wana wa Mungu.

Shetani ndiye kiongozi wa kunakili kazi za Mungu. Siku zote anashindana na Mungu akitumia kazi zake akijifanya ni zake ili yeye apate heshima kama za Mungu. Shetani alishapata adhabu yake kutokana na hii kazi yake ya kunakili. Sasa usikubali wewe kuwa namba mbili wa kuadhibiwa na Mungu kama shetani kutokana na kutumia kazi zake na kujidai ni zako. Adhabu yako itafanana na ile ya Lucifer alivyofukuzwa mbinguni. Wewe isije ikakupata hiyo.

Maoni


Ingia utoe maoni