Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Novemba 08, 2021

Jumatatu, Novemba 8, 2021.
Juma la 32 la Mwaka

Hek 1:1-7;
Zab 138:1-10;
Lk 17:1-6


KUWA CHANYA KATIKA ULIMWENGU HASI

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza tunasikia kuhusu habari za hekima. Ni tunu ambayo kila mmoja anapaswa kuitamani, ni tunu itokayo kwa Bwana, hekima ni Takatifu. Hekima huja pale tunapojizatiti na kuanza kupendelea mema, kutenda haki. Waweza kuwa na elimu kubwa sana, au na vipaji vizuri sana lakini kama hupendelei haki na mema hakika huwezi kuwa na hekima. Hivyo tujifunze kupenda mema.

Mara nyingi kuchagua kutenda dhambi kunachaguliwa kwa kirahisi zaidi kuliko kutenda mema. Dhambi inachaguliwa zaidi kuliko mema. Siku zote kitu rahisi kina gharama kubwa. Hivyo duniani ni wachache tu wenye hekima. Hivyo tujitahidi kuendelea kupenda kutenda mema. Vipaji vyetu, kazi na vyeo vyetu vimeshindwa kuisaidia jamii kwa sababu ya kupendelea kuvutiwa na urahisi wa kutenda dhambi kuliko mema. Tupendelee yaliyo mema.

Hivyo tuangalie kazi tunazofanya, lazima nihakikishe kwamba kazi zetu tunazitenda kwa wema na haki. Kama ni wafanya biashara, tusiwauzie watu bidhaa mbovu au fake. Tupendeleee kuwafanyia watu vitu vizuri.

Katika somo la injili, Bwana Yesu anaelezea juu ya adhabu itakayotolewa kwa yeyote mwenye kumkwaza aliye mdogo. Adhabu yake ni kufungiwa jiwe shingoni na kutupwa baharini. Adhabu hii inafanana na ile aliyopewa joka pale alipokuwa muasi mbinguni. Alitupwa chini na kao lake kuondolewa (Uf 12) na hivyo hakuna hata alama yake iliyosalia.

Adhabu ya mtu anayekwaza wadogo nayo ni kufungiwa jiwe ili naye apotee ili asije akaacha kitu cha kuendelea kukwaza watu waache kumfuata Kristo.

Hivyo tuogope dhambi ya kukwaza wenzetu. tukiendelea kukwaza adhabu yake ni kali, yenye kufanana na ile aliyopewa mkuu wa uovu wote, lile joka kubwa (Uf 12). Tuwe mfano mzuri kwa wadogo zetu. tuwaoneshe mfano mzuri. Tuongee nao maneno mazuri, tuepuke kutumia lugha mbaya kati yao, tusiwafundishe ukatili, matusi au uchafu wote. Kila mmoja ampende aliye mdogo.

Pia Yesu anasisitiza juu ya kusamehe kwamba tusichoke kuwasamehe wenzetu. Wapo wenzetu watakosea mara mia, na watakuja kila wakati kuomba msamaha lakini tusichoke na yule anayetukosea na kuja kila siku kuomba msamaha. Wanadamu wengi ni dhaifu hivyo tusisite kwenda kuomba msamaha kila tunapowakosea wenzetu na sisi tusichoke kutoa msamaha kwa wenzetu. Kristo hutoa msamaha kwetu kila siku. Nasi tusiache kutoa msamaha kwa wenzetu.

Maoni


Ingia utoe maoni