Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Novemba 03, 2021

Jumatano, Novemba 3, 2021.
Juma la 31 la Mwaka

Rom 13: 8-10;
Zab 112: 1-2, 4-5, 9 (K) 5;
Lk 14: 25-33.


GHARAMA YA KUWA MFUASI!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana asubuhi ya leo linaendeleza kile tulichoanza kusikia siku ya jana kwamba mwaka wa kanisa unaelekea ukingoni na masomo tunayoanza kuyasikia hasa somo la injili ni kuhusu nyakati za mwisho na maandalizi yetu kwa maisha ya baadaye. Katika injili hii, Yesu anaweka dhahiri juu ya kinachohitajika kwa yeyote yule anayetaka kuwa mfuasi wa Yesu-ni lazima ajikane nafsi yake achukue msalaba wake na kumfuata. Anayetaka kuwa mfuasi wa Yesu lazima akubali hata kumchukia baba yake na mama yake na hata nafsi yake. Ni lazima ukae chini na upime je kweli nitaweza?

Ndugu zangu, Yesu anatumia maneno yote haya tena yakiwa ni makali kabisa, yanachoma sana na kwa baadhi yetu tunaweza kufikiri kwamba yanakwaza kuonyesha jinsi ilivyo makini kumfuata Yesu. Itakubidi upingane na mitindo mbalimbali na kasumba mbalimbali na hata mila na desturi mbalimbali za kabila lako, familia yako na wenzako. Itakubidi ubakie siku zote ukitetea ukweli wa injili na hapa ndipo kasheshe itaanza, nakwambia utagombana na baba, ndugu, na hata watu wa kabila lako.

Kwa mfano, kwa ukristo itakulazimu uwe na mke mmoja-hii kwa baadhi ya makabila hutaeleweka, itakubidi uache mila kama kuridhi mke wa kaka yako na kuzaa naye-hapa unaweza usieleweke kabisa, itakukataza usipige ramli au kufanya mazindiko mbalimbali. Nakwambia hapa mtanishuhudia kwani wanaokataa kufanya mambo haya unakuta familia au ukoo wote unakutenga. Haukuelewi kabisa. Naamini kuna wale wanakaresmatiki wamekumbana na kitu kama hiki. Kuna sehemu fulani ukikataa kushiriki katika matambiko au mazindiko yanayofanywa na familia unatengwa. Na hapa unabii wa Yesu unatimia.

Halafu nakwambia ukishikilia msimamo wako wa dini hata ukiwa kazini kwako, nakwambia unashangaa unaona hata baadhi ya watu, wale unaofikiri kuwa ni rafiki zako, waliokutegemea upige nao dili na wewe usipige, nakwambia wanakutenga. Hawakualiki kwenye masherehe yao tena, wanakuacha huko, wanakusema, na wewe kama huna moyo unaweza kwenda kuwaomba msamaha ili uungane nao.

Huu ndio ukristo ndugu yangu. Kumfuata Yesu, msimamo wako wa kiimani umesababisha utengwe, uonekane kama nuksi kwa wenzako. Hili ni fundisho kwetu ndugu zangu ili pale mambo kama haya yakitokea, tusishtuke au kuogopa sana kiasi cha kwenda kuwaomba msamaha na kujiunga na makundi yao. Wewe bakia na Mungu na pia fuata kile anachosema Paulo katika somo la kwanza kwamba usiwe na deni jingine kwa mwenzako isipokuwa kupendana. Wewe bakia katika kuwapenda hata kama watakuchukia wewe usiwatendee ubaya wowote au kuwalipiza. Jua kwamba Yesu amewahi kuyatabiri haya na injili ya leo ikutie moyo hasa wakati huu ambapo kanisa hututafakarisha juu ya ujio wa mwisho wa maisha yetu.

Maoni


Ingia utoe maoni