Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Novemba 01, 2021

Jumatatu, Novemba 1, 2021.
Juma la 31 la Mwaka

SHEREHE YA WATAKATIFU WOTE

Uf 7:2-4, 9-14;
Zab 23:1-6;
1 Yn 3:1-3;
Mt 5:1-12


WATAKATIFU: WITO WA PAMOJA WA KUWA MTAKATIFU

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo tunaadhimisha sherehe ya watakatifu wote na masomo yetu yanatualika vyema kwenye kuitafakari siku hii ya leo. Zaburi yetu ya wimbo wa katikati inatuambia juu ya kizazi cha wamtafutao Bwana na watakaoruhusiwa kupanda mlima wa Bwana. Waliofanikiwa kuupanda huu mlima wa Bwana kuna Abrahamu, Musa na Elia. Walipanda mlima wa Bwana na kukutana naye na kuongea naye na kupewa faraja kubwa.

Habari za watakatifu tunaowasikia katika somo la kwanza nao wamepanda mlima wa Bwana na sasa wamekutana na Bwana na kufarijiwa naye na kuoshwa kila chozi machoni mwao. Hawa walivaa mavazi meupe yaliyooshwa kwa damu ya mwanakondoo na walipokuwa duniani walikubali kutiwa muhuri wa mwanakondoo na mkombozi na leo wameshika matawi mikononi wakimshangilia mfalme wao Yesu Kristo.

Sisi ndugu zangu tufuate njia yao. Kwanza tujikubali kutiwa chapa ya mwanakondoo tukiwa hapa ulimwenguni kwanza kwa kukubali kubatizwa, kupokea sakrament mbalimbali. Hapa tunajitia chapa na kujifunga kwamba sisi ni wakristo. Kila mmoja leo aone umuhimu wa sakramenti katika kumtia chapa hii. Tuongeze bidii kwa pale tulipoacha kuzipokea na tuache kasumba za kuwaacha watoto wetu bila kubatizwa miaka na miaka.

Malaika wa somo la kwanza anatudhihirishia kwamba siku hii ya watakatifu ni siku inayoonyesha kupewa tuzo kwa wale waliopitia katika dhiki kuu na Yesu analidhihirisha katika injili anapofundisha juu ya heri leo. Maisha ya heri katika ulimwengu yanaonekana kuwa maisha ya kupitia katika dhiki kuu. Waliomaskini wa roho-wasiongangania vitu au kuonyesha upole na kuishia kudhulumiwa, wanaotafuta amani na kupigania haki. Watu wa namna hii wameishia kudhulumiwa ndani ya ulimwengu huu.

Waliopigania haki baadhi wameishia kuuawa na maadui. Hawa ndio waliopita katika dhiki kuu na hakika leo wamepewa tuzo. Yesu hakika anakumbuka hata unywele wa kichwani mwetu. Chochote tulichokitoa kwa ajili yake hakika atatutunza na kuturudishia. Tusiogope kujitoa kwa ajili ya wengine. Tusiogope kupitia katika dhiki. Waliopitia dhiki ndio wanatukuzwa leo. Sisi tusitake kupendwa na kuchekewa na watu ili kubembeleza dhambi. Hawa waliopendwapendwa waliishia kukutana na Lucifer kule motoni.

Heri na baraka za Mungu kwa sikukuu ya somo wa kila mmoja wetu leo. Tutamani utakatifu tukimbie dhambi.

Maoni


Ingia utoe maoni