Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 26, 2021

Jumanne, Oktoba 26, 2021,
Juma la 30 la Mwaka

Rom 8: 18-25;
Zab 125: 1-6 (K) 3;
Lk 13: 18-21.


UFALME WA MUNGU NDANI MWETU


Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Ekaristi takatifu asubuhi ya leo. Tunaendelea na barua ya mtume Paulo kwa Warumi na leo katika somo la kwanza Paulo hazungumzii tena masuala ya neema bali anazungumzia juu ya tumaini la kufanywa kuwa wana wa Mungu ambao viumbe vinalisubiria. Paulo anaangalia viumbe vyote na kuona kwamba kila kimoja kina tamaa, tamaa ya kuishi milele, kila kiumbe kinasikitishwa na kifo. Paulo anasema hata sisi ambao tumemvaa Kristo ndani yetu tunalia pia, tuna maumivu, tuna tamaa kubwa, tunatamani tukombolewe, tuondoshwane na kifo, tuondoshwane na mauti ya duniani na kuwa wana wa Mungu. Hivyo, Paulo anatuambia tuendelee kutumaini tu na tutumaini kwa saburi na kwa sababu tumaini letu ni la kitu ambacho hatujakiona bado, yafaa kuwa na Imani na saburi. Hivi ndivyo vitakavyotufikisha.

Yesu katika injili analipatia maelezo tumaini hili linalosisitizwa na Paulo katika barua ya Warumi anapofananisha ufalme wa mbinguni na chembe ya haradali na chachu iliyochachusha unga mwingi. Hapa anadhihirisha kwamba ufalme wa mbinguni upo ili ukue, uwafikie watu wengi na kuwakaribisha wengi kama chembe ya haradali inavyozalisha mti unaoweza hata kuwakaribisha ndege nao wakafurahi.

Huu ni ujumbe wenye matumaini makubwa kwamba Mungu anataka wote tuwe watoto wake ili tuondokane na kuoza ambako Paulo amekuzungumzia katika somo la kwanza.

Huu ndio ujumbe wa matumaini Yesu na Paulo wanaoutoa. Nasi tunaalikwa kuwa watu wa kupeleka ujumbe wa matumaini kwa wenzetu. Hakikisha kwamba hata kama unakwenda kumuonya mwenzako, ujumbe wako lazima uwe na matumaini. Humuonyi na kumwachia matusi na majeraha bali unamwacha katika tumaini, katika mstari. Hivyo tujifunze kupeleka habari za matumaini kwa wenzetu. Usipeleke laana, matusi, au mabomu ya kuangamiza roho yake na kuiacha katika uchungu.

Kingine ukipewa wajibu fulani, hakikisha unakua, watu wanapata hata nafasi ya kuja na kupumzika hapo. Kama wewe ni mama ntilie au mpishi hotelini, fanya hiyo kazi vizuri, pika vizuri, watu waje wafurahie chakula chako, wawe kama hawa ndege wanaokuja kupata pumziko katika haya matawi ya mmea wa haradali. Usifanye vitu vyako kwa kulipua kiasi kwamba hakuna hata anayefurahia unachoandaa wewe. Hii ni muhimu sana ndugu zangu. Fanya vitu vyema na vifanye kwa moyo wote. Vipaji alivyokupa Mungu vitumie vizuri watu wapate Baraka na kumuona Mungu kwa kupitia wewe, usitumie kipaji vibaya alichokupa Mungu, usikitumie kuunguza watu bali kipaji chako kitoe kivuli cha watu kupumzikia na kuona faraja na kumtukuza Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni