Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 27, 2021

Jumatano, Oktoba 27, 2021,
Juma la 30 la Mwaka
Warumi 8:26-30
Zaburi 13:3-6
Luka 13:22-30

akukinge na majambazi wakati wa usiku

Karibu wapendwa kwa adhimisho la Misa takatifu. Ni dhahiri kwamba mwanadamu wengi hawajui kile wanachohitaji na hivyo hawajui kukiomba. Ni Roho tu anayejua yaliyo ya muhimu kwetu na hivyo hutusaidia kuyaomba hata pale tusipoyaomba. Hakika tunasaidiwa na Roho katika maombi yetu kwani yapo mengi ambayo hatuyaombi lakini tunashangaa tunayapata.

Ebu jiulize, jana usiku kabla ya kulala ulikumbuka kumwambia Mungu akusaidie ili usiamke ukiwa mgonjwa, au akukinge na majambazi wakati wa usiku? Sasa inakuwaje wengi wetu tumeamka bila kukumbwa na majanga kama haya. Hakika tunaweza kushuhudia kwamba yupo Roho anayetusaidia katika kuomba kwani wanadamu wengi hatujui kuomba ipasavyo. Wengi tunaomba tukifikiria ya sasa tu, tukitawaliwa na mitazamo finyu. Roho anakamilisha pale tulipoachia. Hivyo siku ya leo tumshukuru Roho kwa namna anavyochukuliana nasi, kwa jinsi anavyotuonea huruma na kutusaidia.

Somo hili kwa hakika Paulo anaonesha uhusiano wa karibu uliopo kati ya Mungu na wanadamu kwamba hakika sisi ni wa thamani kubwa machoni pake, na tayari amekwishatuahidia makubwa tangu awali na anataka tuyamiliki hayo makubwa na urithi wetu aliotuandalia hakika ni mkuu.

Kila mmoja wetu ajiulize, je, kwa hakika ninaufaidi urithi ulioletwa na Kristo? Je, ni vilema vipi vinavyonifanya nishindwe kuufaidi urithi wangu? Zipo kasumba na dhambi zinazotuthoofisha na kutufanya maskini, kutufanya tuishi kwa wasiwasi, na kuwazuia wengine kutupatia msaada. Hizi zinanifanya nishindwe kuufurahia urithi wangu. Lazima niachane na madhambi na kasumba hizi.

Yesu katika Injili anatueleza kwamba kutakuwako na hukumu ya mwisho na waliomtii Bwana kwa hakika watatunzwa. Watakaotunzwa ni wale wenye kupitia katika njia nyembamba. Njia nyembamba ni njia ngumu, yenye kujinyima na wengi hawaichagui. Anayeichagua njia hii huenda kinyume na mitazamo ya wengi kwani wengi wanaipenda njia pana. Njia pana humaanisha mafundisho, maeneo, bidhaa, viongozi na mitazamo yenye kupendelewa na wengi katika jamii. Mengi yanayopendwa na dunia ni hatari kwa maendeleo ya kiroho na kimwili.

Nikiona ukumbi au bar, au msanii au kiongozi anayependelewa sana na dunia mara nyingi aweza kuwa kikwazo kwa maendeleo ya kiroho na kimwili. Hivyo tuwe tayari kuchunguza mafundisho, maeneo na watu wanaopendwa na dunia

Maoni


Ingia utoe maoni