Alhamisi, Oktoba 21, 2021
Alhamisi, Oktoba 21, 2021.
Juma la 29 la Mwaka
Rom 6: 19-23;
Zab 1: 1-4, 6 (K) Zab 40:5;
Lk 12: 49-53.
MOTO USAFISHAO
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Ekaristi takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza kutoka katika barua ya mtume Paulo kwa Warumi. Hapa tunamkuta Paulo anaendelea na ule ujumbe wake wa neema ya Mungu iliyopo katika Kristo Yesu na leo anatoa ujumbe mzito kwa Wakristo wale wa Roma ambao hawakuwa Wayahudi, wale waliokuwa kutoka mataifa mengine. Hawa anawaaambia kwamba wao mwanzoni waliishi katika dhambi kubwa sana. Wao walikuwa wanaabudu mizimu, waabudu sanamu, wazinzi wakubwa, wabinafsi, waonevu wa wanyonge, wachoyo wakubwa, wakioa wanawake wengi, wakiolewa na wanaume Zaidi ya mmoja. Hayo ndiyo yaliyokuwa maisha yao na kwa kipindi hicho, hakuna aliyewaambia kwamba walichokuwa wanatenda ni dhambi.
Wao waliona tu mambo yote ni sawa na kila mtu alikuwa anakazania tamaa zake za mwili azitimize. Hilo ndilo lililokuwa lengo lao. Na hawakujilaumu hata kidogo. Mwenye nguvu alifaidi tu.
Lakini kwa sasa baada ya kuipokea injili-kwa kweli wakikumbuka matendo yao ya zamani, nakwambia wanajionea huruma wao wenyewe, wanajicheka na wengine wanataka kulia. Wanajionea aibu jinsi walivyoishi katika ujinga. Na Paulo anawaambia kwamba faida ya kuishi haya maisha mapya waliyoyapata sasa, faida yake itakuwa ni kuupata utakatifu. Hiki ndicho ndugu zangu Paulo anachofundisha siku ya leo. Na ujumbe huu wa Paulo kwa Wakristo wa Roma unapewa angalizo na Injili ya leo Yesu anaposema kwamba amekuja kuleta Mafarakano ulimwenguni.
Hii inamaanisha kwamba hawa wakristo wa Roma kwa kuikumbatia imani na hii neema ya Kristo, haimaanishi ati watakuwa wanaishi salama bila fujo yoyote. Nakwambia watafanyiwa fujo Zaidi na kwa sababu kuna watakao kataa kuwapokea na kuyaona maisha yao kama ni ushamba. Watachukiwa na watu, baadhi watakataa kuwaalika katika sherehe zao au hata kuwapa michango mbalimbali. Watu watawaita ni vimbelembele, wanafiki.
Lakini nakwambia ndugu yangu ukiona rafiki yako, kaka, dada au mtoto wako anakukataa, anakuletea fujo kutokana na misimamo yako, kwa sababu wewe unampinga na unachambua kila asemacho na kumrekebisha-usiogope. Huu ndio ule moto uliokuja kutupwa huku duniani na Yesu. Wewe bakia kwa Yesu na msimamo wako.
Usijiingize kwa mambo ambayo yatakuletea aibu ati kisa unabembeleza urafiki. Huku kutakushushia heshima yako, utakuja kudharaulika na kila mtu, hakuna atakayekuja kuomba hata ushauri toka kwako. Nakwambia mwishoni utakuja kujionea aibu wewe mwenyewe. Hivyo, bakia katika jambo la haki na kweli japokuwa utatengwa na wenzako wewe usiogope.
Maoni
Ingia utoe maoni