Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 19, 2021

Jumanne, Oktoba 19, 2021,
Juma la 29 la Mwaka

Rom 5: 12, 15, 17-21;
Zab 40: 6-9, 17 (K) 8,9;
Lk 12: 35-38.


KUWA MWEPESI KUMKARIBISHA YESU


Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Mungu katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza linalotoka katika barua ya mtume Paulo kwa Warumi. Na leo tunaendelea kusikia ujumbe juu ya ukuu wa neema ya Mungu-jinsi ilivyo kuu. Na leo katika kuwafundisha wakristo wa Roma juu ya ukuu wa Neema hii, Paulo anatoa miongoni mwa kauli zilizo kuu kabisa katika barua yake kwa Warumi-na kauli hii imetumiwa sana na mababa wa Kanisa kuelezea juu ya ujio wa dhambi ya asili duniani.

Paulo anasema “kwa njia ya Adamu, dhambi iliingia duniani na kusababisha kifo kwa kila mwanadamu, kila aliyekuwa mzao wa huyu binadamu wa kwanza yaani Adamu. Lakini kwa njia ya Kristo, neema iliingia duniani, wokovu, uliingia duniani na sasa kila amwaminiye huyu Kristo, hawapatwi tena na dhambi na kifo bali wanaondolewa dhambi zao na kushinda kifo na kuupata uzima wa milele.

Ndugu zangu, hili ni miongoni mwa mafundisho makuu kabisa ya mtakatifu Paulo juu ya ukuu wa neema ya Kristo na huruma yake. Na mababa wengi wa kanisa kama akina Mt. Augustino wameyatumia sana kuonesha ujio wa dhambi ya asili duniani na hivyo umuhimu wa ubatizo unaomfanya mtu mwanachama wa Kristo katika kuiondoa dhambi hii. Paulo anaonesha kwamba kwa ujio wa Kristo, neema za Mungu zimeongezeka zaidi na Zaidi lengo likiwa ni kupambana na dhambi iliyokuwa inaongezeka na kumtesa mwanadamu zaidi na zaidi. Hivyo, Paulo anataka kuwaambia Warumi kwamba wamwamini Yesu, wamwekee matumaini yao yote-hakika wataokoka kwani hakuna Zaidi ya Yesu.

Ndugu zangu, ujumbe huu wa kuwa na imani na kumwamini Yesu unasisitizwa tena zaidi katika injili yetu. Injili yetu inaelezea juu ya habari za mwisho wa dunia, ile siku ya mwisho atakapokuja Kristo kuuhukumu ulimwengu. Anasema kwamba heri yule atakayemkuta anakesha, amefunga viuno vyake tayari kwa ujio wa Bwana, yule ambaye hawatesi wale watumwa walioko chini yake bali atakutwa akiwatumikia.

Ndugu zangu, Yesu anaposisitiza juu ya kukesha-hamaanishi eti akukute kanisani, chini ya msalaba au tabernacle umelala pale unasali. Anachomaanisha ni mtazamo wa maisha atakao kukuta nao wakati huo, juu yake yeye na juu ya wenzako.

Je, atakukuta katika majivuno makubwa ukiiona dunia hii kama mali yako na wengine wote ni kenge tu? Atakukuta katika ubinafsi mkubwa wa umimi tu, yaani ukihangaikia maslahi yako tu, ukiwa na vitu ulivyowaibia wenzako na kuwaacha katika majonzi makubwa? Atakukuta katika kuwasaidia mayatima wangapi na maskini wangapi? Atakukuta katika ndoa kamili, ukiwa na upendo kwa mke wako au mume wako? Hivi ndivyo atakavyo kuhukumu navyo.

Hata ulizia magari mangapi uliyokuwa nayo au nyumba yako ilikuwa kubwa kiasi gani au ulisoma chuo gani. Hayo hapana. Basi tuachane na ule moyo wa majivuno na ubinafsi tunaposubiria mwisho wetu. Tuwe na moyo wa kinyenyekevu Zaidi.

Maoni


Ingia utoe maoni