Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 20, 2021

Jumatano, Oktoba 20, 2021.
Juma la 29 la Mwaka

Rom 6: 12-18;
Zab 124: 1-8 (K) 8;
Lk 12: 39-48.


UFUASI: WITO WA KUWA MWAMINIFU, SI KUFANIKIWA!

Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika Zaburi yetu ya wimbo wa katikati toka zaburi ya 124 tunakutana na ujumbe usemao msaada wetu u katika jina la Bwana. Na hakika kama Bwana asingalikuwa upande wetu, adui zetu wangalikwisha tuangamiza na kuturarua.

Adui anayezungumziwa leo ni dhambi ya asili; huyu ndiye adui mkubwa aliyetuzunguka, aliyetaka kuturarua lakini Bwana alikuja upande wetu na kutupatia ukombozi na kuzifanya nafsi zetu ziondoke katika mtego kama ndege. Sisi tumekwisha kombolewa katika dhambi ya asili. Kila kiungo chetu, na mwili wetu tayari umekombolewa na ndiyo maana utafufuliwa ile siku ya mwisho.

Basi tusikubali kuvirudisha tena viungo vyetu katika dhambi. Macho, mikono, midomo na masikio yetu vimtangaze Bwana Mungu wetu. Tuvitafutie viungo hivi mazingira rafiki, tukae katika maeneo ambayo yataweza kuvilisha viungo hivi na kuvifanya vimtangaze Bwana.

Wengi wetu tunavichosha viungo hivi kwa kukaa katika mazingira yenye uasherati, yenye filamu chafu, yenye kutuangamiza zaidi.
Tukivitumia tena viungo vyetu kwa ajili ya dhambi tunakuwa kama mtoto anayetumia mali aliyopewa na Baba yake kuwalipa majambazi wanaotaka kumwangamiza Baba yake. Tushirikiane na Bwana wetu.

Katika somo la injili, Bwana Yesu anazungumzia juu ya ujio wa nyakati za mwisho. Anatuambia kwamba tujiandae, tuzipende nafsi zetu na roho zetu zaidi kuliko mwenye nyumba alindavyo mali yake ili isiharibiwe na wezi. Wengi wetu tunajali mali kuliko roho zetu. Lakini tunapaswa kuhakikisha kwamba pale ilipo na nafsi zetu ndipo na roho zetu zinapopaswa kuwapo.

Tumtumainie Mwenyezi Mungu na tumkabidhi roho zetu ili zipate kuwapo katika mikono yake salama.

Maoni


Ingia utoe maoni