Jumatatu, Oktoba 18, 2021
Jumatatu, Oktoba 18, 2021.
Juma la 28 la Mwaka
Sikukuu ya Mt. Luka Mwinjili
2 Tim 4:10-17;
Zab 144:10-13, 17-18;
Lk 10: 1-9
KUBEBA USHUHUDA WA YESU KRISTO
Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Ekaristi asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya mtakatifu Luka mwinjili. Yeye hakuwa mtume bali alikuwa mfuasi wa mitume na alimfuata sana Mt. Paulo na injili yake ameiandika kutokana na habari juu ya Yesu alizozisikia sana toka kwa Paulo. Ukweli wa suala hili tunalisikia katika somo la kwanza ambapo Paulo anamuonesha Luka kama mfuasi wake mwaminifu aliyebaki naye hata kipindi kile alichokuwa gerezani. Alikaa na Paulo na huko alipata kujua habari nyingi kumhusu Yesu. Yeye hakuwa Myahudi bali alikuwa mkristo toka Antiokia na hivyo katika injili yake, amejitahidi kuonesha namna jinsi Yesu anavyojihusianisha na watu wa mataifa, jinsi Yesu alivyowapatia nafasi watu wa mataifa katika suala la wokovu.
Mfano: katika Lk 7:1-10, Luka anaeleza habari ya akida wa Kirumi aliyeonesha imani kubwa, Imani ambayo Yesu anaisifu na kusema kwamba hajawahi kuiona imani kubwa kama hiyo katika Uyahudi wote. Katika Luka 10:25-37, Luka anaonesha jinsi Msamaria alivyoweza kuwa na upendo kuliko Wayahudi (kuhani na Mlawi walimwacha yule aliyepigwa na wanyanganyi lakini Msamaria alimsaidia. Halafu tena yule Msamaria aliyeponywa kati ya wale kumi ndiye yeye tu aliyekuja kutoa shukrani).
Ndugu zangu, yote haya ni Luka akionesha kwamba Mungu hana ubaguzi na watu wa mataifa wana nafasi kubwa katika ukombozi. Hawajatupwa.
Uelewa huu ulimpatia moyo sana Luka. Hivyo aliamua kuyatolea maisha yake katika kuitangaza injili na kuiandika ili watu wasi ishie katika injili potofu. Ukweli ni kwamba hii sehemu ya injili ya Luka tunayoisoma leo kutoka sura ya 10:1-9, mwinjili huyu aliishi na ilimtia moyo sana. Hii ni kwa sababu yeye alitambua fika kwamba yeye si mtume lakini anajua kwamba Mungu bado alihitaji wafanyakazi shambani mwake. Hivyo hakuogopa kumfuata Yesu. Alijitoa sadaka kuhakikisha kwamba watu wanapata injili safi juu ya Yesu. Alisafiri na Paulo, wakavumilia mateso, Wayahudi wakawakimbiza, Paulo akafungwa gerezani lakini yeye yupo naye, Paulo anachapwa viboko na yeye anaona yote hayo lakini hakukata tamaa. Alizidi kusafiri naye ili apate kuwaandikia watu injili safi. Mwishowe, mwinjili huyu aliifuata ile njia aliyopitia Paulo. Naye alikufa kifo dini. Ama kweli aliishi kile alichoandika katika injili ya leo.
Ndugu zangu, toka kwa mtakatifu huyu tunajifunza mengi. Kwanza mtakatifu huyu alikuwa msomi. Alikuwa daktari. Lakini aliona usomi wake si kitu mbele ya Yesu. Hii ni changamoto kwetu ndugu zangu. Tutumie elimu yetu kumtangaza Kristo na sio kuwasumbua watu na kuwatenga wengine. Kuna watu ambao wanasema, hasa wanafunzi, nikifaulu vizuri, nikipata one safi, siendi utawani. Nikipata three, naenda. Wengine wanashauri watu kwamba maksi zako hazitoshi chuo kikuu. Nenda usista au ubruda. Tafakari unataka kumwambia Mungu nini? Angalia sadaka yako isije ikawa kama ile ya Kaini! Usiwe kama mtu anayetoaga chenchi kama sadaka. Sadaka ya jumapili iandae kabisa. Si unaenda kutoa mabaki/ chenchi.
Hivyo msifuate mkumbo unaosema kwamba waliofaulu vizuri hawaendi utawani. Hapana! unadanganywa, tena waliofaulu wanahitajika ili walikuze kanisa la Mungu, ili kuelezea kwa ufasaha mafundisho ya Kanisa, wanahitajika sana hawa watu.
Kingine-kama wakristo tutambue kwamba hata sisi ni wamisionari. Kwa ubatizo wetu ni wa misionari. Sasa jiulize-kwa kipindi chote ulichoishi hadi sasa-umefanya umisionari gani? Ni kipi chema ulichofanya cha kuweza kumwambia Mungu kwamba mimi nimefanya umisionari. Ni umisionari gani unafanya wewe? Angalia tangu asubuhi hadi jioni ukilinganisha lugha mbaya (matusi) na maneno ya kimisionari- yapi mengi? Ukilinganisha dharau ulizowafanyia watu na umisionari uliofanya kipi kikubwa?
Ujumbe mwingine ni kwa wale wanaokimbia rafiki zao wakati wa shida. Mt. Luka katika somo la kwanza alibaki na Paulo hadi kifungoni na baadaye aliachiliwa huru na shughuli kuendelea. Sasa wewe ukisikia mume mgonjwa, au kafilisika umeshakimbia au rafiki yako kafilisika au kaumwa, au kavunjika umeshamkimbia. Tabiaa hii sio nzuri. Mwige Luka.
Maoni
Ingia utoe maoni