Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Oktoba 16, 2021

Jumamosi, Oktoba 16, 2021
Juma la 28 la Mwaka

Jumamosi kumbukumbu ya Bikira Maria

Rom 4: 13, 16-18;
Zab 105: 6-9, 42-43 (K) 8;
Lk 12: 8-12.


IMANI YA JASIRI


Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza kutoka katika waraka wa mtume Paulo kwa Warumi. Hapa tunamkuta Paulo akieleza juu ya umuhimu wa imani katika maisha ya mkristo na anatumia mfano wa Abrahamu na kusisitiza kwamba Abrahamu ni Baba wa wote wanao amini, wote walio na Imani ndio tu wanaoweza kuitwa watoto wa Abrahamu kwa sababu Abrahamu alihesabiwa haki na Mungu kwa kuonyesha Imani.

Torati aliyopewa kuishika ilikuja baadaye, ilikuja baada ya yeye kuonyesha Imani. Hivyo, yeyote ajiitaye kwamba ni mtoto wa Abrahamu yafaa aonyeshe imani kubwa pia, kwa sababu Baba yake ambaye ni Abrahamu alikuwa mtu wa imani kubwa na pia kwa sababu watoto wa Abrahamu wameahidiwa mbingu, wote wanaoamini wanakuwa watoto wa Abrahamu nao wataiona mbingu.

Ndugu zangu, Injili yetu ya leo inaendeleza ujumbe huu kwa kuonyesha namna tunavyopaswa kuiishi Imani yetu. Imani yetu inapaswa isimuonee aibu Yesu mbele za watu, lazima kumshuhudia mbele za watu na yeye atakushuhudia mbele ya malaika mbinguni. Yesu anaendelea kusema kwamba atakaye mkufuru Roho Mtakatifu huyo hatasamehewa. Ndugu zangu kumkufuru Roho Mtakatifu ni kuukataa ule mwaliko unaoletwa na Roho Mtakatifu wa kumwamini Yesu upate wokovu. Kumkufuru Roho Mtakatifu ni kuukataa mwaliko huu na kumwambia sitaki, siuhitaji, acha nibaki peke yangu.

Kwakweli ndugu yangu mtu aliyefikia kikomo hiki kwa kweli ni mtu aliye na kiburi cha hali ya juu kabisa-wale wanaona kwamba kinachosemwa na Yesu ni ujinga mtupu, hakinisaidii, hana lolote, dharau kubwa-kama wale Wafarisayo waliomuona Yesu, amemtoa pepo wa ajabu kabisa aliyemfanya mtu bubu na kiziwi-wao wakakataa kuukiri ukweli wa Mungu, walisema-anatoa kwa nguvu ya beelzebul, yaani walimsifu shetani na kumwona ni wa maana zaidi kuliko Yesu.

Ndugu zangu, masomo haya yanayomengi yakutufunza. Cha kwanza ni juu ya wivu. Ndugu zangu, Yesu alitoa ujumbe huu mzito kwamba atakayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa baada ya Wafarisayo kumdharau Yesu na kila alichokuwa anafanya na kuona kwamba shetani ana nguvu hata kuliko Yesu.

Yote haya yalisababishwa na wivu-lengo ni kwamba Yesu asiaminike. Na sisi tuepuke dhambi za namna hii. Wivu utatufanya hata tushirikiane na wezi, wauaji, na watu watendao kila uovu lengo likiwa ni kuwadidimiza tu wale wanaofanya vizuri kuliko sisi. Nakwmbia tuepuke dhambi hizi. Kama upo tayari kushirikiana hata na wauaji kumwangamiza mwenzako au kumfanyia ubaya-jua kwamba na wewe unaelekea kumkufuru Roho Mtakatifu kama ilivyotokea kwa wale Wafarisayo walipoona Yesu kaponya mtu.

Cha pili ni kwamba tujifunze kukubali. Tujue kwamba kuna watu maishani wanaotuzidi kimaarifa au kinyanja mbalimbali. Na kama mtu amekuzidi katika Nyanja Fulani, shirikiana naye, jiunge naye, usimwangushe chini, usitafute kumpindua.
Kingine lazima kujifunza kutokumwonea Mungu aibu. Dhihirisha Imani yako.

Kama kuna uovu unafanywa na watu fulani, sema, usikae kimya tu. Ukiona kwamba kuna watu wanaonewaga na wengine, sema, saidia. Kama wewe ni polisi na mwenzako anaibiwa kila siku, saidia. Usione aibu. Mke wako au mume wako anamtesa mfanyakazi wa ndani mtetee, na dhihirisha Imani yako kwa kuwa mtetezi kama Kristo. Kwa Imani ambayo tunaipata kwa njia ya ubatizo sisi ni manabii, nabii haongei ili kuwafurahisha watu bali anaongea kwasababu ndio ukweli wenyewe. Watoto wako wenye lugha mbaya waonye usione aibu, kama wanapotoka kimaadili wasaidie usione aibu, kemea dhambi, kama Yesu alivyo waambia Wafarisayo waache maisha yasio mpendeza Mungu. Kwa njia hii utakuwa unaishi Imani yako ndani ya Kristo

Maoni


Ingia utoe maoni