Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 13, 2021

Jumatano, Oktoba 13, 2021,
Juma la 28 la Mwaka


Rom 2: 1-11;
Lk 11: 42-46.

Wengi wetu tuna vidhambi vyetu vya sirisiri,
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo linatuongoza kutafakari kwamba Bwana atamlipa kila mmoja sawasawa na haki yake. Ndivyo zaburi yetu ya wimbo wa katikati inavyotueleza. Bwana hatazami urafiki, yeye huchunguza mioyo na akili ya mwanadamu. Wapo kati yetu wenye kujitangaza kuwa wenye haki mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu hatatazama wingi wa kelele yetu, bali atatazama haki kamili, tuliyo nayo sisi kama sisi.

Paulo katika somo la kwanza anatoa ujumbe mkuu kuhusu kutoa hukumu kwa mwingine. Anasema kwamba waanadamu dhaifu kama sisi hatuna uwezo wa kumhukumu mwenzetu na kumwita kuwa asiye na haki kwa sababu nasi muda sio mrefu tutaangukia katika dhambi ile ile, au udhaifu ule ule ambao mwenzetu anautenda. Waswahili wanasema hujafa hujaumbika, hivyo hatuwezi kujitangazia chochote au kujihalallishia chochote kuhusu sisi tukijiona kwamba sisi ni wema au la.

Paulo anaandika ujumbe huu kuhusu baadhi ya Wayahudi ambao walijivuna na kuwaona watu wa mataifa mengine kama wasiostahili kuupata wokovu. Paulo anakazia mkazo kwamba Bwana ni hakimu mwenye haki. Wayahudi walipewa upendeleo wa kuwa taifa teule, hivyo hawapaswi kubweteka kwa nafasi hiyo, bali wanapaswa kutumia nafasi hiyo kujiweka karibu zaidi na Mungu na kuonesha heshima zaidi kwake.

Nasi ndugu zangu twaweza kubarikiwa zaidi na Mungu lakini tujifunze kunyenyekea zaidi na zaidi. Mungu anapotubariki kwa mara moja, sisi tusianze tena kuonesha mzaha mbele yake, kadiri unavyobarikiwa, ndivyo uzidi kumheshimu Mungu zaidi. Wapo waliowahi kubarikiwa lakini kila walipobarikiwa, ndivyo walivyozidi kukaa mbali na Mungu kwa kuzidisha anasa, majivuno na matukano.

Katika somo la injili, Bwana Yesu anazidi kuendeleza makemeo yake dhidi ya Wafarisayo. Kwa hakiki ilibidi Yesu afanye hivi kwa sababu Wafarisayo walikuwa kioo cha jamii lakini kama wangaliachwa bila ya kukemewa, hakika wangaliiharibu jamii kwa maneno yao na mipango yao michafu. Yesu anawaita kwamba wapo kama makaburi yaliyofichika, ambapo kwa juu yanaonekana kuwa masafi lakini kwa ndani kumejaa uozo.

Yesu anaonesha uovu wao hadharani ili wabadilike na waijenge jamii. Nasi tunahitaji mtu atakayesaidia kuuweka uovu wetu mbele ya macho yetu, atakayetukemea kutokana na uovu wetu ili nasi tupate kubadilika. Wengi wetu tuna vidhambi vyetu vya sirisiri, hivi ni vibaya sana. Vitatuangusha sana. Tunahitaji atakayetukemea ili tupate kubadilika na kuwa wema zaidi. Nasi tukipata anayetukemea kutokana na uvou wetu, basi tukubali kubadilika ndugu zangu na kuwa wema zaidi na sio kupambana naye na kutaka kuteketeza maisha yake. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni