Alhamisi, Oktoba 14, 2021
Alhamisi, Oktoba 14, 2021.
Juma la 28 la Mwaka wa Kanisa
Rom 3: 21-30;
Zab 130: 1-6 (K) 7;
Lk 11: 47-54.
UFUNGUO WA MAARIFA!
Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Ekaristi asubuhi ya leo. Leo neno la Mungu tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza linalotoka katika barua kwa Warumi. Hapa tunamkuta Paulo akiwaeleza Warumi kwamba sote tunaokolewa kwa neema ya Mungu na si kwa matendo ya sheria. Hii ni kwa sababu sote tu wadhambi, Wayahudi na watu wa mataifa pia. Sote tu wadhambi na tunahitaji neema ya Mungu. Na neema hii inapatikana kwa Yesu peke yake na si kwa mwingine. Hailetwi na matendo ya sheria kama ya kuosha mikono hadi kwenye kiwingo, au kutahiriwa. Neema hii inaletwa kwa kumwamini Yesu.
Ndugu zangu, hiki ndicho Mafarisayo katika injili walichokosa. Wao walisisitiza mno matendo ya sheria. Hata na wazee wao pia. Na alipotokea nabii akitaka kuwafundisha hata juu ya namna ya kumwabudu Mungu kwa utakatifu, wao hawakuwa tayari kupokea kwani walitegemea naye nabii afuate kile wanachotaka wao, kile wanachojua wao wenyewe. Hawakutaka nabii awafundishe mtindo tofauti na wao. Kwa sababu hiyo waliishia kuwaua manabii wote na Yesu anawaambia hata nyie mtaishia kufanya kama babu zenu kwa sababu hamjabadilika, bado mnaishi kama wao kwa hiyo hata kama mnajidai kusikitika kwa kilichofanywa na babu zenu, bado mtaendelea kufanya hivyohivyo-mtazidi kuwauwa manabii na mtazidi kujifungia wenyewe msiingie katika mlango wa hekima na kuokolewa.
Ndugu zangu, Wafarisayo na taifa zima la Israeli walishindwa kumpokea Yesu na manabii kwa sababu hawakujiachia moja kwa moja kwake. Wao walithamini vionjo vyao zaidi. Walitaka kumfundisha nabii na sii nabii awafundishe. Ndio maana waliishia kuwauwa wote. Nasi ndugu zangu tutambue kwamba kama hatutajiachia mbele ya Kristo, tutajikuta kama hawa Wafarisayo tu walioshindwa kumpokea Yesu. Kama utakuja kwa Yesu ukitaka kuja kumfundisha kipi akupe na namna ya kukupa, vyote hivi unamfundisha namna ya kukupa, nakwambia mwisho wa siku utashindwa kukutana na Yesu na utaishia kupoteza imani tu au kubakia mtu wa kulalamika.
Ndugu yangu, Mungu hafundishwi bali wewe kubali kufundishwa. Hiki ndicho walichokosa Wayahudi.
Kingine, tuwe tayari kuwakubali hata wale waliochini yetu kiuchumi na kimaarifa. Kitu chema sio kwamba kila mara kitaletwa na mtu mwenye maisha safi. Hata watu maskini wanaweza kutuletea habari njema. Manabii wengi walikataliwa kwa sababu walikuwa watu maskini maskini. Wao walitegemea nabii awe mtu mashuhuri, kiongozi hodari. Hivyo nabii maskini yeyote hakupokelewa vizuri kwenye ujumbe wake.
Sisi nasi tunaweza kuishia kudharau maneno ya padre fulani kwa kisingizio kwamba huyu namfahamu tangu akiwa mseminari ataniambia nini? Baba yake mbona namfahamu kamaskini ka mwisho! Kama una hali hii ndugu yangu badilika. Hata wakati mwingine unashindwa kupokea ujumbe kutoka kwa padre au mtu fulani kwasababu tu ni rafiki yako na unamfahamu, angalia sana, yeyote aweza kukuletea maneno ya kinabii ya kubadilisha maisha yako, acha kubagua au kujiona siwezi kufundishwa na huyu au unajichagulia wa kukufundisha! Jifunze kupokea watu kwa unyenyekevu na uwe tayari kusikiliza na kuanza maisha mapya, usiwe kama Mafarisayo ukakosa neema ya Mungu.
Maoni
Ingia utoe maoni