Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Oktoba 11, 2021

Jumatatu, Oktoba 11, 2021.
Juma la 28 la Mwaka

Rom 1: 1-7;
Zab 98: 1-4 (K) 2;
Lk 11: 29-32.


ISHARA YA YONA

Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana kwa siku ya leo tunaanza kwa kuliangalia somo la Injili kutoka Injili ya Luka. Katika Injili hii tunamkuta Yesu akitoa lawama kali kwa baadhi ya watu waliokuwa wanamsikiliza. Chanzo cha lawana hizi ni kejeli zilizotolewa na hawa baadhi ya watu wakimwambia ati anatoa pepo kwa nguvu ya Beelzebuli-hawa watu hawakuikubali ishara hii na hivyo walitaka atende zaidi-atende ishara kubwa ya kimbinguni mbinguni hivi. Sasa Yesu leo anakasirika na kuwaambia kwamba hiyo inatosha na kama bado wanategemea nyingine basi wasubirie tu ile ya Yona.

Ndugu zangu ishara ya Yona ni ishara ambayo wewe mwenyewe unachagamka kufanya kitu kwa ajili ya wokovu wako na si kusubiria mtu akufanyie kitu. Wale watu wa Ninawi waliposikia tu yale mahubiri, walichangamka. Hivyo Wayahudi nao wangetakiwa wakisikia tu maneno ya Yesu nao wachangamke na kutubu kwa sababu Paulo katika somo la kwanza anatuambia kwamba Injili, habari njema aliyofundisha Yesu iliahidiwa na Mungu tangu zamani kupitia manabii wake na Injili hii ni Yesu mwenyewe na kwa njia yake tunafanywa kuwa wana watakatifu wa Mungu.

Hivyo Paulo anawahimiza Warumi wampokee Yesu na hapa watapokea utakatifu.

Lakini kwa sababu wale wa Ninawi walitubu na hivyo kusamehewa dhambi zao, japokuwa wao ni wamataifa, wao watajikuta wanaingia mbinguni na kukalia vitu kumi na mbili vya kabila la Israeli na kuwahukumu waisraeli waliokataa kutubu. Paulo katika somo la kwanza anataka Warumi wampokee Yesu ili kisiwapate kilichowapata baadhi ya wana wa Israeli.

Ndugu zangu, injili hii ni onyo kubwa kwa baadhi yetu tunaomchukulia Yesu kimzaha mzaha. Tunaona kwamba anachotutendea Yesu hapa duniani ni cha kawaida sana. Tunataka atende zaidi. Labda siku moja niamke nikute pochi yangu imejaa pesa tu, au magari ya kutosha. Hapo ndipo nitakapo mwamini. Nakwambia ndugu yangu tukienda na mawazo haya kwa Yesu tutaishia kumkana Yesu. Mawazo ya namna hii hayajengi Imani ya mtu. Ndugu zangu kwa sasa Yesu ameshatuachia sakramenti. Hii ndiyo ishara ambayo kwayo twaweza kumkuta Yesu. Ridhika na hiyo. Ukiwa na tamaa ya kutafuta ya ziada utaishia tu kuhama makanisa na mwishowe utapoteza Imani yako tu.

Kingine ndugu zangu ni juu ya toba. Nakwambia phakuna kitu kinatufaa sisi kama toba. Maishani mwetu tuthamini toba. Toba ndiyo itakayorudisha uhusiano wako na Mungu. Toba ndiyo itakayotupeleka kwa Mungu. Asiyethamini toba kama baadhi ya makutano tunaowasikia katika injili ya Yesu nakwambia atakosa yote. Toba itakuunganisha na Mungu. Jifunze thamani ya toba.

Kingine ni juu ya wivu. Ukiwa na wivu hutakaa uweze kuona jambo zuri toka kwa mwenzako. Wivu uliwafanya baadhi ya Wayahudi wakubali hata kushirikiana na muovu ili wamwangushe Yesu. Walikubali hata kutukuza nguvu za shetani ili wazififishe za Yesu. Hawa baadhi ya makutano waliokuwa wanamsikiliza Yesu walimjibu jibu baya namna hii kwa sababu tu waliona kwamba huu muujiza mkubwa hivi hauwezi kufanywa na mtu kama huyu. Ndugu zangu, hata sisi tabia zetu za namna hii zimewafifisha sana wenzetu. Baadhi yetu tumekubali kushirikiana hata na maadui ili kuwafifisha baadhi ya ndugu zetu. Kuna ndugu zetu tumedidimisha mawazo yao, utaalamu wao, tukavifukia hata vipaji vyao ili tu wabakie hukohuko. Tabia hii haitatufikisha popote ndugu zangu. Kama umefanya hivyo tubu anza maisha mapya.

Maoni


Ingia utoe maoni