Jumanne, Oktoba 12, 2021
Jumanne, Oktoba 12, 2021,
Juma la 28 la Mwaka
Rom 1: 16-25;
Zab 19: 2-5 (K) 2;
Lk 11: 37-41.
KUONDOA UNAFIKI WOTE!
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa Takatifu. Neno la Bwana katika siku ya leo tunaanza kwa kuiangalia injili. Hapa tunamkuta Yesu akilaumiwa kwa kula bila kunawa mikono kwa kadiri ya desturi za Wayahudi na aliyemwalika anajisikia vibaya-anasema huyu mtu tabia zake hazitamfikisha kwa Mungu, zitamfikisha kwa muovu.
Hivyo aliyemwalika anajiona kana kwamba anatenda jambo kubwa kwa sababu anamuokoa Yesu ili asije akakosa wokovu. Yesu anamgeukia na kumwambia kwamba huwezi kuuacha moyo wako katika msitu wa dhambi kama za dhuluma, uonevu, uzinzi halafu ukategemea kuokolewa kwa kushika desturi ya kuosha mikono au kikombe. Utoe moyo wako katika huo msitu wa dhambi kwanza hasa zile dhambi zako ufanyazo sirini.
Ndugu zangu, jambo hili ndilo lililokuwa sehemu kubwa ya utume wa Yesu-kuwaelewesha watu juu ya mtindo mwema wa kumwabudu Mungu. Mtindo waliokuwa nao haukufaa ndugu zangu, huu mtindo wa kusisitizia juu ya matendo ya nje nje na kuuacha moyo wako kwa mbali katika dimbwi la dhambi. Ndio maana katika somo la kwanza Paulo anasema kwamba haionei aibu injili kwa sababu ndiyo nguvu yenye kumpatia wokovu kwa yeyote mwenye kuamini.
Lakini watu waliicha injili na kwenda kuviabudu viumbe, kuhangaikia matendo ya mwili na kuacha kumwamini Mungu wa kweli. Wakafuata wanavyoambiwa na vionjo vyao vya mwili na mwishowe wakashindwa kumjua Mungu wa kweli na pale walipomtambua walishindwa kujua namna sahihi ya kumwabudu na kuishiwa kutawaliwa na vionjo vya mwili.
Ndugu zangu, masomo haya yanatoa ujumbe mzito sana kwetu. Kati yetu wanatumia mambo matakatifu kuficha uovu wetu. Ni kama jambazi anayejidai kabeba msalaba kumbe ndani yake kaficha bunduki au kisu. Wapo kati yetu tunangangania kuwa viongozi kanisani au kutoa sadaka kanisani au kuonekana katika vyama vingi vya kitume tukifikiri kwamba ukishajiingiza katika mambo haya basi wokovu unao.
Wewe huoni namna unavyowajibi watu vibaya ofisini mwako, au kuwatukana wafanyakazi wako au kuwadhulumu watu mali zao au hata kuomba rushwa kama ni vya hatari kwako. Vya hatari ni kutokutoa sadaka kanisani au kukosa uongozi kanisani. Nakwambia ndugu yangu badilika. Imani ya namna hii haikufikishi mbali. Au mwingine anajipa matumaini ati nikidhulumu mtu halafu nikitoa hapo kidogo kwa ajili ya sadaka au fungu la kumi mambo yataenda. Nakwambia ndugu yangu unajindanganya. Fedha ya dhuluma inarudishwa kwa mdhulumiwa. Ukitoa sadaka kutoka kwenye mfuko wa dhuluma unalaaniwa Zaidi. Usifikiri kwamba itakupatia Baraka. Hivyo tuepuke kutumia mambo matakatifu kuficha maovu yetu.
Maoni
Ingia utoe maoni