Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Oktoba 09, 2021

Jumamosi, Oktoba 9 2021.
Juma la 27 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mama Bikira Maria

Yoel 4: 12-21
Zab 97: 1-2, 5-6, 11-12 (K) 12;
Lk 11: 27-28.


ULIMWENGU UNAOISHI NDANI YA MAMA MARIA


Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Nabii Yoeli anazungumzia juu ya ujio wa nyakati za mwisho. Hukumu inaelezwa kwamba itafanyika katika bonde Jehoshapati. Hili ni Bonde ambapo Mfalme Jehoshaphati wa Israeli aliwateketeza wafalme watatu walionyanyuka kuipiga Israeli-Mfalme wa Edom, Moab na Edom. Hawa walinyanyuka kuipiga Yuda, taifa takatifu la Mungu lisilo na hatia lakini wakaishia kuangamia katika bonde la Jehoshaphati.

Hivyo Bonde hili limechukuliwa kuwa kama sehemu ya hukumu ambapo Mungu huamua kati ya mwenye haki na mtesi wake, mwenye kuonea na mwenye kuonewa. Na siku zote Bwana atampatia mwenye haki ushindi kama alivyowapatia Yuda chini ya mfalme Yehoshaphati.

Sisi tunaposikia ujumbe huu tujifunze kupatana na watesi wetu kabla ya kufika kwa hakimu. Tujifunze kuomba msamaha, ukweli ni kwamba ipo siku ya hukumu, matendo yetu yote tuliyotenda katika giza yatawekwa hadharani. Kila mmoja leo aangalie mambo anayoyafanya katika siri na kuyaacha kwani mambo haya ndio sababu ya kuangamia kwake, na hakika ataangamizwa kama hawa wafalme watatu walipoanguka katika bonde la Yehoshaphati.

Yesu katika injili anapongezwa na kina mama waliosikia ujumbe mzuri toka moyoni mwake. Hakika mama Maria alipata sifa kubwa pale maneno haya yaliposemwa kwa Yesu. Nasi tuungane na mama huyu katika injili kumwambia Yesu namna hii, hakika mama Maria naye anapata sifa sana.

Pia tumheshimu mama Maria, yeye ndiye aliyemnyonyesha mtoto huyu, yaani Yesu Kristo. Pia kila mmoja wetu ajitahidi kuishi maisha mazuri ambayo yatawapatia wazazi na walezi wetu sifa kama Yesu anavyompatia mama Maria leo sifa. Wazazi na walezi wetu hujisikia vibaya ikiwa kama wale waliowafundisha waliishia kuwa wezi, na wanyanganyi au wasioambilika. Tujitahidi kuwa watu wenye kuambilika ili basi tuwapunguzie na vipressure wazazi wetu.

Maoni


Ingia utoe maoni