Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Septemba 20, 2021

Jumatatu, Septemba 20, 2021.
Juma la 25 la mwaka

Ezra 1: 1-6;
Zab 126;
Lk 8:16-18


WEWE NI NURU: ANGAZA
Ndugu zangu wapendwa, karibuni katika adhimisho la ekaristi asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi yetu ya leo. Leo tunaanza kusoma kitabu cha Ezra ambacho huelezea habari ya wana wa
Israeli wanaotoka uhamishoni Babeli. Tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza linalotoka katika kitabu cha hiki. Hapa tunakutana na simulizi zuri kabisa, la ajabu na la matumaini. Israeli anatangaziwa kutoka
utumwani Babuloni.

Mji wa Yerusalem pamoja na hekalu lililobomolewa na mfalme Nebukadneza
unaahidiwa kujengwa. Israeli anapokea msaada mbalimbali kutoka hata kwa wapagani wakalijenge hekalu
na mji mtakatifu wa Yerusalem. Ndugu zangu, wana wa Israeli waliweza kufadhiliwa na Mungu kiasi hiki kwa sababu waliitumia ile adhabu waliyopewa na Mungu ili kujisafisha. Walitumia adhabu ya uhamisho kama fursa ya kutubu na kuacha dhambi na hivyo Mungu aliwafadhili na kuwaonea huruma.

Ndugu zangu, tunachojifunza hapa ni kwamba kweli Mungu ni Baba mwema, ukimlilia, ukimpigia magoti hata kama una dhambi kiasi gani hata kuacha.

Mada hii inaendelezwa katika injili ya leo. Tutasikia injili ikisema kwamba aliyenacho
ataongezewa lakini asiyenacho hata kile kidogo anachofikiria kuwa nacho atanyanganywa. Fundisho tunaloweza kuoanisha hapa ni kwamba yule anayeshirikiana na Mungu, Mungu humwongezea lakini yule asiyeshirikiana naye hata kile kidogo alichokuwa nacho atakipoteza.

Hapa tuna jambo la kujifunza ndugu zangu kama wanafunzi. Unapotoa muda wako, kipaji chako kwa ajili ya Mungu, kwa ajili ya kuwahudumia wenzako-nakwambia mtu wa namna hii utashangaa anang’aa tu, anafaulu tu. Lakini wale
wanaofichaficha, wanaosoma wenyewe, wanaojitenga, wanaoona kwamba kuwasaidia wengine ni mzigo-utashangaa kwamba hawa siku zote wanafeli tu, wanaamka asubuhi kusoma lakini hakuna kitu, wanapitwa tu.

Nakwambia ndugu yangu uliyeko hivi badilisha njia. Injili ya leo inakuambia hakuna siri ambayo itafichika, kubali kuwa taa-yaani kuwa tayari kusaidia, kutoa ushauri, msaada kwa mwenzako kadiri ya uwezo wako.

Unachokificha kitakuja kutambulika siku moja tu na hapo utaumbuka. Ukimsaidia mwenzako hupotezi. Wema unaomtendea mwenzako utarudishiwa na Mungu. Kwa wale wenye changamoto mbalimbali tusisite kumlilia Mungu. Yeye hakika hatatuacha pale tunapoomba kushirikiana naye. Atatuongezea kile kidogo tulichonacho.

Maoni


Ingia utoe maoni