Jumanne, Septemba 07, 2021
Jumanne, Septemba 7, 2021,
Juma la 23 la Mwaka
Kol 2: 6-15;
Zab 144: 1-2, 8-11;
Lk 6: 12-19
KUUNGANIKA NA MUNGU
Karibuni sana wapendwa wangu kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza, Mt. Paulo anaendelea kuwasihi Wakristo wa Kolosai kwamba watetee uhuru wao. Anawaeleza kwamba wamekombolewa kwa damu Azizi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hivyo wanapaswa kuutetea uhuru wao. Hivyo wasitekwe tena na mahubiri ya wanadamu au wanafalsafa waliojiona kuwa na hekima na ujuzi wa maneno na hivyo kumwacha Kristo. Wajue kwamba Kristo ni wa muhimu sana maishani mwao, wasikubali kupotoshwa na mahubiri, tamaa au ujuzi wa yeyote.
Ujumbe huu uliwahusu Wakolosai ambao kwa hakika walikuwa wanayumbishwa na wanafalsafa wa Kigiriki, ujuzi wao wa maneno uliwayumbisha sana. Pia wengi kati ya Wakolosai waliwakwa na tamaa za mambo ya dunia kiasi cha kushindwa kuona ukuu wa Kristo maishani mwao.
Somo hili litoe funzo kubwa kwetu. Wengi wetu tunayumbishwa kirahisi na maelezo ya wahubiri kiasi cha kusahau ukuu wa imani yetu. Wapo walioasi imani yao kwa kanisa katoliki baada ya kukutana na wahubiri wenye hila, na ushawishi mbaya. Tunapaswa kuelewa kwamba shetani huwatumia wanadamu wenzetu, hasa wale walio maarufu kuuangusha ulimwengu pia. Shetani hutumia hata vifungu vya Biblia ili kutaka kutuangusha. Shetani alipomjaribu Yesu, alitumia maandiko matakatifu ili apate kumwangusha lakini hakufanikiwa.
Sisi tutambue kwamba Kristo wetu ni mkuu kuliko wahubiri wetu. Wahubiri waweza kutumika kama mdomo au mkia wa shetani wenye lengo la kuwaangusha watu katika shimo la shetani. Hivyo tuwe makini na yeyote mwenye kutumia ujuzi wa maneno ili kutuyumbisha. Mhubiri wa kweli anahubiri kwa nguvu ya Roho Mtakatifu na Roho Mtakatifu hahitaji ujuzi wa mwanadamu ili kufikisha ujumbe wake. Ujumbe wake hufikishwa kwa nguvu ya Roho mwenyewe. Sisi tuwe makini na wahubiri, hasa wale wenye kutumia ujuzi wa elimu yao na ujuzi wa maneno yao. Hawa waweza kutumiwa na shetani kuuangusha ulimwengu. Mhubiri wa Kweli atambue ukuu na maongozi ya Roho, na si ujuzi wa elimu.
Yesu katika injili anawaponya watu mbalimbali wanaokuja kwake kuomba uponyaji. Wengi kati yao walioponywa ni wale walionyanyuka na kwenda kutafuta uponyaji toka kwa Yesu. Waliobakia nyumbani, bila kumtafuta Yesu, hawakupata uponyaji. Ni juu yetu kutambua kwamba tunapaswa kunyanyuka na kumpelekea Yesu maombi na mahitaji yetu. Tusitegemee ati wengine watatupelekea mahitaji na shida zetu kwa Yesu. Nao pia wana shida zao. Sisi tunapaswa kunyanyuka wenyewe na kumweleza Yesu shida zetu. Hakika tutaweza kufaidia neema zitokazo kwa Yesu. Ni yule tu anayenyanyuka na kueleza shida zake ndiye hupokea uponyaji. Tusichoke kumkimbilia Mwenyezi Mungu na kumweleza shida zetu zote.
Pia katika injili, Bwana Yesu anawachagua mitume wake. Hawa mitume walikuwa na tabia mbalimbali na hawakuwa wamekamilika, kila mmoja alikuwa na udhaifu wake lakini Bwana Yesu aliwachagua ili kwamba kadiri muda unavyokwenda, wajifunze kwake na wasahihishe udhaifu wao. Sisi katika udhaifu wetu, bado Bwana Yesu anazidi kutuita. Kila anapotuita, tupokee mwaliko wake na kurekebisha mwenendo wetu kama atakavyo Bwana. Tusichoke kujirekebisha.
Maoni
Ingia utoe maoni