Jumamosi, Septemba 04, 2021
Jumamosi, Septemba 4, 2021
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
Sala ya Kanisa (Zaburi)-Juma la 2
Jumamosi kumbukumbu ya Bikira Maria
Kol 1: 21-23;
Zab 54: 3-4, 6, 8;
Lk 6: 1-5
KUONDOKANA NA MZIGO WA MTAZAMO MBAYA!
Karibu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi hii. Neno la Mungu, tutasikia katika injili juu ya nini maana ya sabato na namna sabato ipasavyo kuheshimiwa. Ukweli ni kwamba, wafarisayo walibadilisha maana
ya sabato; Walikuwa na lengo la kutishia watu. Waliiongezea sheria nyingi sana na watu walitegemewa wazishike sheria hizi na ndio tu waliweza kuhesabiwa kwamba wameiheshimu sabato. Mwisho wa siku lile lengo kuu la sabato, yaani kumfanya Mungu atukuzwe na binadamu abarikiwe lilipotea.
Sabato iliishia kuwa kama mchezo wa kuwindana au kukomoana au kujionyesha au kutishiana. Iliishia katika unafiki, katika kujionyesha, katika kumpendezesha mtu fulani na sio Mungu tena. Kwani kulikuwa na kundi la watu ambao kazi yao ilikuwa ni kuwawinda wengine, kutishia wengine, hawajiangalii wao bali wanawinda-yaani watu waishi kama hawa wawindaji wanavyotaka.
Hiki ndicho Yesu anachokataa hapa. Anawambia Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato akimaanisha kwamba sasa wanapaswa kwenda kwake na kupata uelewa wa sabato, sabato yenye upendo, inayomfanya Mungu atukuzwe na si kumtukuza mfarisayo au kutishia watu maisha.
Paulo katika somo la kwanza anatuambia kwamba tuumepatanishwa na
kufanywa watakatifu kwa damu ya Kristo. Hivyo tubakie katika kumwamini Kristo. Hivyo, tumwombe Kristo atufundishe kusali, tusitegemee nguvu au akili za kibinadamu. Mungu atufundishe. Wafarisayo hawakuruhusu kufundishwa na
Mungu bali walitaka sheria zao zitawale na si Mungu. Ndiyo maana walishindwa hata kujua sabato ni kitu gani au hata kujua ni nini cha kufanya katika sabato.
Tujitahidi kuwa wanyenyekevu, sala si ya kutishia au kujipatia utukufu binafsi. Sabato na sala za wafarisayo zilikuwa ni za kutishia. Unapokuwa hata na novena yako jitahidi kusali kwa unyoofu sio wakati wakuwatambia wengine mtu asikuguse una novena yako! Sali kwa nia ya kuomba neema ya Mungu na kuwaombea wengine ujipatie urakatifu na Mungu atukuzwe.
Tuwe watu pia wenye sheria zilizojaa upendo. Tusikazanie kushika sheria wakati unamuona mwenzako anakufa hapo. Sheria ya kwanza kwa Mkristo ni upendo. Tuwekapo sheria zetu tuhakikishe tunatanguliza upendo.
Maoni
Ingia utoe maoni