Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Agosti 27, 2021

Ijumaa, Augusti 27, 2021
Juma la 21 la Mwaka

Sala ya Kanisa (Zaburi) - Juma 1
_______

1 Thes 4: 1-8;
Zab 96: 1-2, 5-6, 10-12;
Mt 25: 1-13
_______

TAA IKIWAKA KWA “MWANGA WA UKARIMU”
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, Bwana Yesu anasisitizia juu ya kukesha kwa kutoa mfano wa wanawali 10 ambapo watano walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye hekima. Wale wenye hekima walikuwa wamejiandaa kila wakati, waliheshimu ujio wa Bwana arusi, mawazo yao yote yalielekezwa kwa huyu Bwana harusi ili ajapo asipate kuaibika; akute wanawali wa kumchezea na kumulikia na hivyo kujipatia heshima mbele ya bibi Harusi.
Lakini wale wasio na hekima walihangaika na mambo yao wenyewe, mawazo yao yalikuwa mbali kabisa na Bwana harusi, hawakujali na pia hawakuwa na kujali kwamba ajipatie heshima au akose, walielekeza mawazo yao katika ubinafsi wao. Mwishowe Bwana harusi anaingia na hivyo hawampokei.
Tukio hili linatufundisha mengi hasa kwa nyakati zetu. wengi wetu tupo kama hawa wanawali wapumbavu, wengi wetu hatumpatii Mungu nafasi, hatumwaliki mioyoni mwetu kama walivyofanya wale wanawali waliokuwa na hekima. Waliokuwa na hekima walimwaza Bwana harusi kwa masaa yote. Wengi wetu tunajiwaza sisi wenyewe na mipango yetu, muda wa sala wa kuongea na Mungu tayari tumekwishaufupisha, sala zetu tunasali kwa haraka, kwenye kusaidia tunasaidia kwa kutoa kile kilichokibovu au kile kilichozidi, na kwenye kusali, tunasali kwa kipindi kile tupatwapo na matatizo kama ya ugonjwa au kufukuzwa kazi. Wakati mambo yakiwa mazuri, Mwenyezi Mungu anatupwa pembeni. Hapa ni kuwa wapumbavu.
Tujitahidi kuhakikisha kwamba kamwe hatumsahau Bwana harusi wetu, yaani Yesu, macho na mioyo na fikra zetu tuzielekeze kwake. Hapa tutaweza kweli kumpokea ile siku ya mwisho.
Katika somo la kwanza, Paulo anatueleza tuishi wito wetu kama tulivyoitwa kama wakristo; tuepuke kuwa kama hawa wanawali wapumbavu. Paulo anasema tuepuke matendo kama ya uasherati na tuichukulie miili yetu katika utakatifu na heshima. Tuepuke tamaa, tupambane na kilema hiki, na tusimnyanyase ndugu yetu yeyote.
Ujumbe huu ututie moyo ili basi tuwe kama wale wanawali wenye taa zenye mafuta. Tuepuke kupoteza muda katika simu huku tukiongea maneno yasiyofaa au ujumbe usiomsaidia mwenzetu. Afadhali tutumie muda wetu kwa ajili ya kumtumikia Mwenyezi Mungu au kumsaidia mwenzetu. Pia tuepuke kutumia rasilimali zetu katika ulevi na uasherati. Hapa ni kama kubeba taa inayofifia. Tubebe siku zote taa iliyojaa mafuta, yenye kupambwa na matendo yetu mema. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni