Jumanne, Agosti 24, 2021
Jumanne, Agosti 24, 2021,
Juma la 21 la mwaka
Sikukuu ya Mt. Bartolomayo, Mtume
Ufu 21: 9-14;
Zab 144: 10-13, 17-18;
Yn 1: 45-51
NJOO NA UONE: KUKUTANA NA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya mtakatifu Bartholomeo Mtume. Huyu ni mtume ambaye habari zake basi tunazisikia kwenye somo la injili akiitwa kwa jina la Nathaniel. Yeye kama tunavyoona katika injili, alikuwa Myahudi, aliyekuwa amezoea tamaduni za kiyahudi na za mtaani kwake, akiamini kwamba kuna maeneo fulani hasa upande wa Galilaya Nazareth ambapo basi hayawezi hata siku moja kumtoa mtu ambaye kweli ataweza kuja kuwa nabii au mtu maarufu.
Lakini leo anakutana na kitu chema na bora, tena toka Nazareth. Zaidi ni kwamba huyu mtu anakuwa bora na mwema kuliko ilivyokuwa kwa baadhi ya wengine waliotoka hata ile mikoa mingine ya Israel.
Yeye anakutana na Yesu, na kuona ukuu wake, basi anakuwa tayari kumkiri kwamba yeye ni Mwana wa Mungu na mfalme wa Israel. Anabadilika mara moja tofauti na Wayahudi wengine ambao walikataa kuubadilisha msimamo wao juu ya Yesu na kubakia kumwona kama mzushi na kuishia kutokumwamini. Yeye alimkiri Yesu kwa haraka sana na hivyo basi alipatiwa nafasi ya kuwa mtume wa Yesu. Aliahidiwa na Yesu kwamba akiendelea kuamini kama alivyoamini, hakika ataona mengi, ataona malaika wakishuka na kupanda juu ya mwana wa Adamu. Hapa yamaanisha kumuona Yesu katika utukufu wake na yeye basi ataungana kwenye huo utukufu kumtukuza na kumsifu.
Hili linadhihirishwa zaidi katika Ufunuo aliouona Yohane katika somo la kwanza ambapo basi aliweza kuona mji mtakatifu, Yerusalem ya mbinguni ukishuka toka mbinguni wenye utukufu wa Mungu, na ulikuwa na majina 12 ya mitume. Hapa yamaanisha kwamba haya maneno aliyoyasema Yesu, hakika yatatimia kwa huyu mtume kama Yohane alivyokwishafunuliwa tena kwenye haya maono.
Ndugu zangu, mtume huyu alihubiri zaidi kwenye sehemu za Armenia. Mtume huyu kweli alikuwa mtu mnyofu sana. Yeye alieleza kile alichoaminishwa na tamaduni zake, na watu wa mtaani kwake na hata viongozi wake wa kidini kuhusu sehemu za Nazareth kwamba hakuwezi kutoka kitu chema. Lakini basi anapokutana na Yesu toka Nazareth na kujua kwamba kweli ni kitu chema zaidi ya vitu vya Yudea na Yerusalem, mara moja anabadilika na anampokea Yesu na kupata wokovu na hata kuja kuwa mtume. Kweli hakuwa na kiburi.
Wengi wetu tunashindwa kuwapokea wengine kwa sababu ya kiburi, tunakataa kuwapokea hata watu ambao wangetusaidia na kwenda kukimbilia kwa wasioweza kutusaidia kutokana na majivuno, wivu na kiburi. Shirikiana nao watakuinua. Hata kama ni darasani-ukiona mwenye uwezo Zaidi yako usianze kumnenea mabaya au kumsengenya ili aanguke. Jiunge naye ili na wewe upande juu kimasomo, hata kama ni kazini ukiona yule mwenye ujuzi na maarifa Zaidi yako-hata kama katokea sehemu maskini au ovyo-jiunge naye akukuze. Ukweli ni kwamba nchi ya America iliweza kupata maendeleo makubwa kwa sababu ilikuwa ikiwaona watu wenye vipaji, mara moja inawachukua na kuwaambia wafanye kazi nao-hawakuchagua mtu-awe Mwafrika, Mhindi, Mchina, Muislam wote waliwachukua na kuwaingiza kwenye zile technologia zake na ile nchi iliendelea sana.
Hiki ndicho Bartolomeo anatufundisha leo. Tuache kuwapiga vita wale wenye maarifa na uwezo. Nakuambia na sisi tungekuwa na moyo wa kushirikiana na wakuu kama wanavyofanya waamerika, nasi tungekuwa mbali sana. Bartolomeo alimuona Yesu kuwa mkuu, akashirikiana naye naye akawa mkuu. Nasi tumpokee Yesu, tushirikiane naye, naye atatukweza.
Mji mpya wa Yerusalemu pia una milango mitatu kila upande, kaskazini, kusini, mashariki na magharibi. Hii ina maana kwamba mji huu upo tayari kumpokea mtu yeyote kutoka katika kila pande. Mji hauna ubaguzi. Hili ni fundisho kwetu kwamba injili ya Yesu au kanisa halina ubaguzi kwa mtu yeyote mlango upo wazi kwa kila mtu kutoka katika kila pande na hivyo tusiwe na hali yakuleta ubaguzi katika kazi ya Mungu au katika kanisa. Mlango upo wazi kwa kila pande katika mji huu, hivyo wale wanaofanya jitihada kuingia tusianze kuwapiga vita kwakizingizio cha kutumia ukabila! Kila mmoja ajitahidi kuingia katika mjii huu kiuamini kwani milango ipo wazi pande zote. Tusipoteze muda kuwapiga vita wale wanaojitahidi badala yake sisi tuwe na mashindano yakutafuta utakatifu.
Maoni
Ingia utoe maoni