Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Agosti 23, 2021

Jumatatu, Agosti 23, 2021
Juma la 21 la Mwaka

Sala ya Kanisa (Zaburi) - Juma 1
_______

MASOMO YA MISA
1 Thes 1:1-5, 8-10;
Zab 149:1-6, 9;
Mt 23:13-22
_______

KUONDOA SURA YA UNAFIKI!
Karibuni sana wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Paul anawasifu Wathesalonike. Anawapongeza kwa imani yao ya kuyaacha mambo ya zamani na kupokea upya, upya ulioletwa na Kristo. Walikuwa tayari kuacha sanamu zao, na kumkumbatia Yesu, Yesu Kristo. Sanamu ziliwafanya waishi kwa kudhaniana vibaya wao kwa wao katika jamii yao, zikawafanya waonane maadui wao kwa wao.
Kristo alipoingia, alivunja uadui wa namna hii na kuleta amani. Alitangaza upendo, alileta uelewano, na maisha ya kujitolea baina ya ndugu na wenyewe kwa wenyewe. Paulo anawasifu Wakristo wa Thesalonike kwa kumpokea Kristo namna hii na kumfanya kuwa dira katika maisha yao.
Sisi tujiulize kwa siku ya leo, je, na mimi nimempokea Kristo kama watu wa Thesalonike? Naweza kusifiwa kama Paulo anavyowasifu Wakristo wa Thesalonike? Basi tukubali kuacha maisha yetu ya chuki, au kudhaniana vibaya, au kutokusaidiana sisi kwa sisi. Tuache maisha ya namna hii ndugu zangu. Wengi wetu kwa hakika bado tumeshindwa kuendelea kutokana na matendo ya namna hii. Tukubali kuacha matendo ya namna hii ndugu zangu.
Katika somo la injili, Yesu anawalaumu wafarisayo kwamba wanazunguka kuongoa watu lakini mwishowe yule anayeongolewa anafanywa kuwa mbaya zaidi. Uongofu wao badala ya kuwafanya waache dhambi wanaishia kuwa wabaya zaidi kwa maisha yao. Tujiulize ni kwa nini? Hii ni kutokana na unafiki. Pale wanapomhubiria mtu aongoke, wanajidai kumwonesha matendo mema, lakini akishaingia kwenye system/taratibu zao, hukuta maovu wanayoyatenda kwa ndani na hapa hukwazika na kuwa wabaya zaidi. Hili litufundishe juu ya hasara za unafiki ndugu zangu. Unafiki hautatufanya tuweze kuwaongoa watu, utatufanya tuwafanye watu kuwa wabaya zaidi. Sisi tuache unafiki. Kila mmoja yapo matendo yake mabaya anayoyatenda kisirisiri. Tujifunze kauchana na matendo ya namna hii ndugu zangu kwa sababu ipo siku yatagundulika na hapa yatawakwaza wengi hasa wale wanaotuangalia sisi kama kioo kwao. Kama ni mzazi, mwalimu, au kiongozi yoyote anayehusika na dini ajitahidi kuacha matendo yake ya kinafiki kwani yatairudisha nyuma injili badala ya kuifanya isonge mbele. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni