Jumapili, Agosti 22, 2021
DOMINIKA YA 21 YA MWAKA B WA KANISA
Karibuni ndugu zangu kwenye adhimisho la misa takatifu Jumapili ya leo ikiwa basi tunaadhimisha dominika ya 21 ya mwaka B wa kanisa. Ujumbe wa neno la Mungu bado unaendelea kuongozwa na maneno yetu ya zaburi yasemayo onjeni muone ya kuwa Bwana yu mwema. Haya ni maneno ya mwaliko kabisa, yanayomkaribisha mwanadamu kumwambia kwamba mjaribu Bwana naye utaonja wema wake mkuu, wekeza kwa Bwana nawe hakika hatakutupa. Ni maneno aliyoyaimba Daudi yawe kama ushuhuda kwa watakaomfuata.
Anasema kwamba licha ya kwamba anayemcha Mungu hupatwa na mateso, Bwana hamwachi aangamie, yeye huja na kumwokoa tu wala hatamuacha aangamie milele; atasikiliza maneno yake. Lakini basi uovu huleta maangamizi kwa yule aliyeuchagua lakini wenye kumtafuta Bwana, kila mara watalindwa salama. Haya ni maneno ya kiushuhuda yaliyotolewa na Daudi mwenyewe, anatoa historia ya maisha yake ya kiimani ilivyokuwa sikuzote ikiongozwa na Bwana. Hivyo basi anaalika kila mmoja kuwekeza kwa Bwana. Huu ndio ujumbe wetu mkuu; kuwekeza kwa Bwana nawe hakika utapata kuuonja wema wa Bwana.
Tukianza kwa kuliangalia somo la kwanza, tunakutana na wosia wa Yoshua. Huyu alichukua uongozi wa taifa la Israeli toka kwa Musa. Alikuwa kiongozi hodari sana, asiyekufa moyo, aliyekuwa na ufundi wa vita na Roho wa Mungu alikuwa juu yake, alimtii Mungu siku zote, na aliliongoza taifa hili kwenye magumu mazito kuelekea nchi ya ahadi baada ya kifo cha Musa. Yeye basi aliweza kuvuka ule mto Yordani kwa nguvu kabisa, akapigana akaweza kuiangamiza mji wa Yeriko, umaarufu upo kwenye uwezo aliokuwa nao wa kuweza kulifikisha lile taifa kwenye ile nchi ya ahadi. Alipofika nchi ya ahadi, aligawia kila kabila la Israeli ardhi na watu basi walianza kulima na kupata yale mazao ya kwanza na kuanza kunywa yale maziwa na asali. Kipindi chake, ile mana ilikatika ikawa haianguki tena kwani walikuwa wamekwishafika ile nchi ya ahadi.
Huyu Yoshua aliyaona maajabu yote ya Mungu, tangu ile mana ikianguka, tangu lile agano la mlimani Sinai, tangu alivyoweza kuwanywesha maji kule jangwani, tangu alipokuwa anatembea kule jangwani, jinsi kulivyotokea baadhi ya watu wakamwasi Mungu na kuadhibiwa, jinsi wote waliomtegemea Mungu walivyoweza kuokoka, jinsi Mungu alivyowafadhili. Yoshua aliyaona yote haya. Na hapa aliuona wema mkuu wa Mungu, naye mwenyewe akauonja, alinyeshewa mana akaila, akanywesha maji jangwani, akaongozwa na ile nguzo ya moto, akalindwa na nyoka wa sumu, kweli aliuona wema huu. Yeye basi siku ya leo anakaribia kwenye somo letu, amekwishazeeka, anakaribia kufa na basi anaacha wosia. Anasema kwamba ama kweli mimi nilisafiri na kubarikiwa na Bwana vizuri sana. Kweli nyakati kwa jinsi nilivyokwisha okolewa, sitaweza kumwacha Bwana na kizazi changu chote kimtumikie Bwana.
Yoshua ilibidi atoe maneno haya ya kiushuhuda kwa sababu kulikuwa na kizazi ambacho cha vijana. Hiki kilizaliwa baadaye, hakikuona yale maajabu yaliyofanywa na Mungu kule jangwani, hivyo walikuwa hawana imani thabiti, walianza hata kufuata zile tamaduni za miungu ya kipagani ambayo basi haikuhusika kuwaokoa. Sasa anaona hatari hii anawaambia kwamba kumbukeni kwamba sisi tuliyaona yale makuu Mungu aliyotutendea, tumeokolewa na Bwana, hii miungu mingine haikuwako wala haikuhusika kutupatia hii ardhi, hivyo basi msiinamie, lazima basi mtambue Bwana. Mimi na kizazi changu ndugu zangu tutamtumikia huyu aliyesafiri nasi tangu zamani hizo.
Haya maneno ya kiushuhuda ya namna hii tena tunakutana nayo yakiendelezwa katika injili ya leo. Yesu alikuwa akiwaeleza wanafunzi wake kwa wiki kadhaa sasa juu ya yeye kuwa mkate mtakatifu ulioshuka kutoka mbinguni na kwa namna gani yeye basi ameweza kutuonjesha wema wake. Kwa kitendo chake yeye kujifanya mkate ili sisi tuweze kuula na kutuongoza hadi tuifikie ile nchi yetu ya ahadi. Mkate huu kwetu unakuwa kama ile nguzo ya moto iliyosafiri na wana wa Israeli kule jangwani hadi kuwafikisha kwenye nchi ya ahadi. Walipopata taabu yoyote, walikwenda kwenye hii nguzo ya moto ipate kuwaongoza na kweli ndiyo iliyoweza kuwafikisha kwenye hii nchi ya ahadi. Kama isingekuwa hii nguzo, hakika wangaliangamia kwenye lile jangwa kavu na kame sana.
Ndani ya ile nguzo walichota nguvu ya kupambana na kila aina ya kiu na uchovu wote.
Ndivyo ilivyo kwa Ekaristi. Ni mkate unaopaswa kutuongoza namna hii, kutuonyesha pa kupita na pa kupaepuka jinsi ile nguzo iliyokuwa kwa wale wana wa Israeli. Kweli ni upendo tosha na sisi basI tunaalikwa kuukubali upendo huu. Alikwishawaeleza kwamba yeye ni zaidi ya ile mana na aliwaaalika kwamba waje wamle. Sasa siku ya leo anamalizia fundisho hili juu ya namna yeye mwenyewe alivyokuja
Lakini basi wengi wanaposikia fundisho hili hawalielewi na wengi wanakwazika na kurudi nyuma ikiwepo baadhi ya wanafunzi wake.
Lakini yesu anawaeleza kwamba jamani, acheni kurudi nyuma. Mjue kwamba maneno niliyowaelezeni ni roho na tena ni uzima. Yaani hayo ndiyo ya kufuata. Na Yesu anawaambia wale wanafunzi wake kwamba jamani nanyi mnakwazika na hili? Jamani msikwazike, ninyi ninawategemea sana. Haya ndiyo maneno mnayopaswa kushika. Petro anatokea na kusema hakika tutayashika.
Ndugu zangu, kwenye haya masomo tunajifunza mambo yafuatayo:
Kwanza-ekaristi ni kiini cha maisha ya mkristo. Ni kama ile nguzo ilivyokuwa kwa wale wana wa Israeli kule jangwani. Tunatakiwa tuchote nguvu, uponyaji utoke hapa, tumaini letu litoke hapa, faraja tuipate hapa kama ilivyokuwa kwenye ile nguzo. Kama hadi sasa hatujaweza kuipata faraja toka kwa ekaristi, au matumaini, au nguvu ya kusonga mbele au huoni chochote-basi kuna mahali unapokosea; anza tena upya, au omba kufundishwa upya, mwambie Mungu akujazie tena imani. Kweli ekaristi inapaswa iwe hivyo.
Au ikitokea kwamba umekwenda kuabudu na kutafakari mbele ya ekaristi kama pale St. Joseph halafu unatoka huoni kana kwamba kuna kitu kimekuingia, au hujapata muongozo wowote, hakuna kilichotokea, kweli omba kuanza mafundisho upya au jua kwamba kuna shida kiroho. Yafaa kuomba ushauri tena.
Pili: tumeona katika somo la kwanza kwamba kizazi kilichokosa uzoefu wa mambo makuu aliyoyatenda Mungu kinakuwa rahisi kurubuniwa na kuingia kwenye kutokumheshimu Mungu. Wao walizaliwa na kukuta kwamba wema wa mungu umekwishakuwapo wakaanza kuula tu bila kujua umetoka wapi. Ndivyo inavyotokea kwa siku za leo. Unakuta mzazi aliipata mali yake kwa tabu, alisali akimuomba Mungu, na Mungu amembariki na wewe basi umezaliwa ukaanza kumtukana Mungu. Hapa sio vyema. Wewe ukikuta mzee wako anamali, uliza kwanza, utaona kwmba kweli alionyeshwa wema wa Mungu. Wewe usianze kuula tu bila hata ya kumkumbuka Mungu. Huo ulikuwa ni wema wa Mungu.
Tatu ni kwamba ama kweli siku hizi kumeibuka kundi la wengi wasioona umuhimu wa ekarisit. Ni kwamba watu basi wanakaa miaka na miaka hawafungi ndoa na hawaoni aibu au kuogopa. Wanaona ni afadhali wasipokee ekaristi kuliko waache kuishi uchumba. Hapa ni kama mkataa pema. Ndio maana uhusiano wa namna hii hauwezi kudumu. Hii ni kwa sababu kuishi na mwanadamu mwenzako kwahitaji neema, kwahitaji msaada wa Mungu. Sio kurahisi. Na hivyo basi ni lazima usaidiwe. Lakini cha huzuni ni kwamba ni wachache tu ndio wanaonaga umuhimu wa kitu kama hiki. Wengi tunaona kwamba uhusiano utaongozwa tu kwa nguvu zangu; hapana mambo hayako hivi. Tujitahidi, sala tuzizidishe.
Nne: Yoshua anawaonya wana wa Israel waepuke ile miungu mingine kwa sababu basi wakati wao wanateseka, ile miungu haikuwa karibu yao wala haikuwafahamu, wakati wanahitaji maji kule jangwani na kuona kiu au kupatwa na magonjwa, haikuwa karibu. Hivyo basi waachane nayo na wasije wakamfanya Bwana aonekane ati achukue nafasi ya pili.-Mungu ndiye aliyetuonyesha wema wake tangu tulivyokuwa wadogo. Kwa baadhi yetu, tulianza kuombewa na mama zetu wakituombea kwa sakramenti ya ekaristi kila siku tangu enzi hizo, wengine tulizaliwa kwa shida lakini basi Mungu akaweza kutupigania kwa sababu ya upendo wake. Hivyo ni lazima tumpende huyu Mungu wetu. Tuipende ekaristi iliyoweza kutuongoza na kutupigania hadi sasa. Achana na hivi vimiungu au vidini vingine au virafiki vinavyokufanya ati leo uiache ekaristi au umwache Mungu; usikubali ati urubuniwe na rafiki yako ati anayetaka kukuoa ili uache ekaristi; mwambie kwamba unataka niache ekaristi-wakati nazaliwa, namlilia Mungu ananiokoa wewe ulikuwa wapi? Ni Mungu tu ndiye aliyenipigania, sasa wewe unakuja kwangu kirahisirahisi hivi? Halafu nikufuate na kumwacha Mungu wangu,aliyenipigania wakati wote? Sio kweli.
Kwenye somo la pili tunakutana na barua ya mtume Paulo kwa waefeso na anasisitizia juu ya upendo wa mke kwa mume na mume kwa mke. Basi na iwe hivi kama ilivyoandikwa hapa. Nianze kwa kusema kwamba achana na vitu kama nyumba ndogo; hii ni kwa sababu watakupenda wakati ukiwa na pesa tu. Lakini wakati ule ukiwa maskini unateseka, ni mke wako tu ndiye aliyesafiri nawe. Sasa uteseke hivyo halafu ati unakuja kumpatia huyu nafasi kama hii na kumwacha yule wa zamani mliyeteseka pamoja?
Tutumie mali zetu na vitu vyetu kwa ajili ya familia zetu. Ni vibaya mume kunenepa na mke kakonda kupita kiasi, ni vibaya kwenda kula kwenye magenge halafu nyumbani hutoi kitu, au umenenepa halafu watoto wanakufa. Hili sio sahihi.
Na wanawake akinamama tuache kuiga. Kweli siku hizi maisha yanabadilika na tujiepushe sana na kuiga mitindo mingine. Mzazi, mama yako lazima akuambie maisha yako vipi. Siku hizi unaiga msanii, unataka ndoa yako ifanane naya akina Obama au Diamond-sio sawa, kunahitajika uvumilivu, kusaidiana, tuchume vitu pamoja na si kununiana na kuachana.
Maoni
Ingia utoe maoni