Ijumaa, Agosti 20, 2021
Ijumaa, Agosti 20, 2021
Juma la 20 la Mwaka
_______
Rut 1: 1, 3-6, 14-16, 22;
Zab 146: 5-10 (K) 1;
Mt 22: 34-40
_______
KUMPENDA MUNGU KWA UFAHAMU WETU WOTE
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu; leo katika somo la kwanza toka kwa Rutu tunasikia habari za shida, baadhi ya watu wa Israeli wanakimbia njaa kwenda kutafuta chakula. Tukio hili la njaa lilikuwa gumu na hakika kuondoka kwao toka Bethlehemu kulikuwa kwa kulazimisha. Lakini cha ajabu ni kwamba safari hii inaleta kitu chema kwani huku ndiko Mungu anakowapatia kitu chema, mama wa kimoabu aitwaye Ruthu ataolewa katika Israeli na huyu atakuwa mke wa Boazi, mama wa Obed, baba wa Yesse atakayekuja kuwa baba wa mfalme Daudi. Hakika mipango ya Mungu ni mikuu mno, haieleweki, ndani ya ugumu mwishowe kipo chema ambacho Mungu anataka kuleta.
Moto unapoanza kuteketeza takataka zinazozuia mbegu kuota au mimnea kuota eneo fulani, wakati moto unateketeza, udongo na vyote vilivyoko pembeni hupata ugumu fulani. Lakini baadaye vitu vizuri huota, mimea mizuri huota na kuleta mazingira safi. Sisi tujitahidi tuwe watu wa kujifunza kutafuta wema ndani ya shida. Katika shida kitu chema chaweza kutokea. Hivyo kila tupatapo ugumu, tusifikirie kwamba ugumu utaendelea kwa nyakati zote, Mungu aweza kuleta chema ndani ya ugumu huo kama mimea mizuri iotayo baada ya moto kuteketeza. Tumwombe Mungu neema ya kutafuta chema kipatikanacho ndani ya ugumu na shida. wengi wetu tunakatishwa tamaa na shida na kusahau kwamba ndani ya huo ugumu chema kitatokea.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anasisitiza tena kwamba amri ilyokuu ni kumpenda Mungu na jirani. Mungu astahili kupatiwa nafasi kuu katika shughuli zetu. Tuwe watu wa kuwatanguliza Mungu na wenzetu mbele. Wapo kati yetu ambao mbwa wetu wanapatiwa chakula chema kuliko jirani wanaotuzunguka. Hapa hatutimizi amri hii ndugu zangu. Wapo ambao gari letu likigongwa kidogo tupo tayari hata kuwajeruhi waliofanya kitendo hicho. Hakika mwanadamu anayo heshima na hadhi kuliko mali au magari. Wapo ambao tupo tayari kuwanunulia wenzetu pombe lakini wanapoumwa au kuhitaji pesa ya matibabu hatupo tayari kuwapa. Hapa sio kumpenda jirani. Jirani yetu apewe kipaumbele kuliko yote tuliyonayo. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni