Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Agosti 16, 2021

Jumatatu, Agosti 16, 2021
Juma la 20 la Mwaka

Amu 2: 11-19
Zab. 106: 34-37, 39-40, 43-44 (K) 4
Mt. 19: 16-22

___________________
Ukigusa tutakosana.

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunakutana na wana wa Israeli wakidumbukia katika mateso na matendo ambayo Yoshua kabla ya kifo chake aliwahi kuwaonya kwamba wasiyatende ili basi wapate usalama toka kwa Mwenyezi Mungu.
Ukweli ni kwamba Israeli alisahau na kuonesha majivuno, alisahau kila alichowahi kutendewa, na kilichowafanya wasahau kirahisi ni kwamba walikuwa katika nchi ya ahadi ambapo walikuwa na kila kitu. Walikuwa na chakula, amani na vya kutosha. Hivyo walimsahau Mungu kirahisi sana na kuanza kujishikiza na watu wa mataifa mengine.
Sisi tunaposikia maneno haya, yafaa tutambue umuhimu wa kukumbuka historia ya maisha yetu, historia ya taifa letu na pia ya wazazi wetu. Wana wa Israeli waliokuwa katika nchi ya ahadi waligeukia miungu mingine kirahisi kwa sababu wengi kati yao walizaliwa katika nchi ya ahadi na hawakubahatika kuyaona matendo makuu ya Mungu aliyoyatenda wakati wazazi wao walipokuwa jangwani.
Hivyo pale walipoelezwa historia ya taifa lao, na juu ya ukuu wa Mungu na ulazima wa kuyafuata mausia ya Mungu, wao hawakuheshimu bali walipuuzia na hivyo wakapatwa na magumu tuyasikiayo katika somo la kwanza leo. Mambo ya namna hii yanakipata na kizazi chetu cha sasa ndugu zangu. wengi kati yetu tunapuuzia, tukielezwa kitu na wazee wetu hatuamini, tunajidai kuwa watu wa sayansi, watu wenye kuamini kile tulichoona au kushuhudia kwa macho. Mambo ya namna hii yanatufanya tushindwe kufuata maongozi ya wazee wetu na kubarikiwa. Tujifunze kuwatii wakubwa wetu, na tujifunze toka kwa historia za wazazi, taifa na za maisha yetu kwa ujumla.
Katika somo la injili, huyu kijana anayemfuata Yesu anaonesha hali ya ajabu kabisa. Ni kwa sababu ni mara ya kwanza katika injili ambapo anayekuja kwa Yesu ameshindwa kurudi akiwa na furaha. Amerudi akiwa na huzuni. Hili ni la kushtusha kidogo. Wengi wanaokutana na Yesu wanarudi wakiwa na amani na furaha. Kwa nini huyu alirudi akiwa na huzuni? Ni kwa sababu mbele ya Yesu alikwenda bila kujiachia. Tayari alikuwa ameshikilia maslahi yake, mambo ambayo alimweleza Yesu kwamba ikiwa utayagusa haya tutakosana. Haya mengine gusa, lakini ukigusha haya, tutakosana. Na moja kwa moja Yesu anayagusa na hakika anashindwa kijana anashinda kupokea.
Sisi nasi tuna mambo ya namna hiyo. Yapo ambayo huwa tunasema haya yasiguswe. Ukigusa tutakosana. Mambo ya namna hii hakika ndiyo yanayotuangusha. Tuwe tayari kujichunguza ni mambo ya namna gani na hivyo tupate kuyaachilia. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni