Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Agosti 15, 2021

Jumapili, Agosti 15 2021
Juma la 19 la Mwaka

SIKUKUU YA KUPALIZWA BIKIRA MARIA MBINGUNI

Ufu 11:19, 12:1-6, 10;
Zab 45:9-11, 15 (K) 10;
1Kor 15:20-26;
Lk 1:39-56


MALENGO YA JITIHADA ZETU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo ikiwa leo tunaadhimisha sherehe kubwa katika kanisa; kupalizwa mbinguni kwake Bikira Maria. Hii ni siku ya ushindi mkubwa kwake; Mama yake Mkombozi ametukuzwa. Alivumilia mengi pamoja na Yesu:-tangu akubali kumchukua mimba licha ya kwamba alikuwa na mchumba tayari (hapa alihatarisha maisha yake lakini hakuona shaka, alikuwa tayari kufa kwa ajili ya Yesu), tangu kukimbilia na Yesu Misri, kumtunza na kumtafuta alipokuwa amepotea, halafu Yosefu alikufa mapema na kumwacha mjana na ugumu wa kutunza nyumba yake.
Halafu akaungana na Yesu kwenye utume wake tangu alipokuwa anauanza hadi anakufa msalabani. Akashiriki vyema kwenye kulianzisha kanisa la mwanzo na kuwa mshauri mkuu wa hii jumuiya ya mwanzo ya Kikristo. Hii ndiyo shughuli aliyoifanya Bikira Maria.
Japokuwa kwenye Biblia hakuna maelezo ya moja kwa moja juu ya kupalizwa mbinguni Bikira Maria, ukweli ni kwamba lile kanisa la mwanzo lilishuhudia hili tukio na kutuandikia maelezo muhimu kuhusu mwili wake kutokuoza kaburini. Wao walishuhudia kabisa na hivyo basi walianzisha ibada mbalimbali za Bikira Maria wakimuona Mama Maria kama mwombezi wa kanisa lao la mwanzo. Ukweli ni kwamba lile kanisa la mwanzo lilipata msaada mkubwa sana kwa kumuomba Mama huyu na ibada kwa Mama huyu haikuishia kwenye kanisa la mwanzo tu. Ilieendelea hadi kukaja kuwa na ibada nyingine za Rozari na zote hizo zilizidi kutokea kadiri ya miaka ilivyokuwa inasonga mbele.
Ndugu zangu, tukijaribu kutafakari kuhusu Bikira Maria; jinsi ibada juu yake ilivyoanza na hadi hapa tulipo, kweli bila ya kuwa na upendeleo wowote kweli hatuwezi kusema ati ibada kwa Bikria Maria ni za kutunga tu. Kweli kama haya yote yangekuwa ni hadithi, ungekuta yamekwishatoweka. Lakini cha ajabu ni kwamba kila kukicha, ibada hii ndipo inapozidi kupata nguvu kila wakati. Kweli kwa Imani na msistizo jamani; Mama huyu kweli astahili kuheshimiwa na kupewa nafasi katika kanisa.
Kingine ni kwamba kupalizwa mbinguni Bikira Maria ni nafasi au upendeleo aliopewa yeye kama yeye. Kama kweli aliweza kupendelewa na kuwa mama wa Mungu, basi anaweza kupendelewa na kupalizwa mbinguni na ndivyo ilivyokuwa. Yesu ana uwezo wa kumpaliza na kweli alimpaliza.
Kupalizwa kwake kulikuwa ni kwa faida yetu. Hii ni kwa sababu huko mbinguni anakuwa ni mwombezi wetu na sio kwamba ati huko anakwenda kutesa na kupiga watu. Amepewa nafasi ambayo basi atakuwa mwombezi wa kanisa na taifa kwa ujumla.
Wapo baadhi wanaopinga kupalizwa Mbinguni Bikira Maria. Wanasema haiwezekani. Lakini nawaambieni kwamba Mungu anauwezo wa kumpaliza na ndivyo alivyoweza kufanya. Hivyo basi leo tuongeze ibada kwa Mama yetu. Leo kapalizwa ili akawe mwombezi wetu. Tumwelekee huko basi tuweze kupata msaada na maombezi yake.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni