Ijumaa, Agosti 13, 2021
Ijumaa, Agosti 13 2021
Juma la 19 la Mwaka
Yos 24:1-13
Zab 135:1-3, 16-18,21-22,24
Mt 19: 3-12
NDOA-AGANO LA UPENDO!
Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu siku ya leo. Leo katika neno la Bwana Zaburi ya wimbo wa katikati inatupatia ujumbe kwamba “fadhili za Bwana ni za milele” ni Zaburi inayoyakumbushia matendo ya makuu ya Mungu aliyowahi kuwatendea Israeli maishani ili basi waweze kuyakumbuka na kuona upendo wa Mungu ndani ya maisha yao.
Zaburi hii inatumika kusisitiza ujumbe wa somo la kwanza leo ambapo Yoshua anayakumbuka makuu yote Mwenyezi Mungu aliyowahi kuitendea Israeli tangu mwanzo wao kama taifa. Lengo la Yoshua ni kuwataka wana wa Israeli wautambue ukuu wa Mungu kwani kusahau ya zamani na kufikiria tu ya sasa ndicho chanzo kikukuu cha wana wa Israeli kuanguka. Kwa kipindi hiki, walipoingia katika nchi ya ahadi, walikutana na watu wa makabila mbalimbali, baadhi walikuwa na tamaduni mbaya, zenye kukiuka maadili ya Mwenyezi Mungu.
Baadhi ya wana wa Israeli walisahau na kuanza kufuata tamaduni mbaya za baadhi ya makabili yaliyopakana na nchi ya ahadi na hivyo kusahau upendo wa Mungu.
Huu ni mwaliko na kwetu kwamba tunalo jukumu la kukumbuka matendo makuu aliyowahi kututendea maishani, lazima shida tulizowahi kupata, ugumu tuliowahi kupata, upendo tuliowahi kuoneshwa maishani. Kuacha haya ni sawa na kuikana imani yetu. Hivyo tuwe watu wa kukumbuka. Wengi wetu tumepotoka kwa sababu ya kukosa kuwa watu wenye kukumbuka, tuna tabia ya kufurahia ya sasa bila kukumbuka hali tuliyowahi kuipitia kwa miaka ya nyuma. Tuwe watu wa kukumbuka na kushukuru.
Katika somo la injili, Yesu anasisitiza juu ya utakatifu wa ndoa, kwamba ni takatifu na haipaswi kuvunjwa, kwani imeunganishwa na Mungu, na alichounganisha Mungu, mwanadamu hana ruhusu ya kukivunja. Fundisho hili liingie akilini mwetu hasa kwa baadhi yetu ambao tunatabia ya kupendelea kuingilia ndoa za watu. Tujue kwamba kwa kufanya hivi, tunajipatia laana. Pia litutie moyo wa kuheshimu ndoa hasa kwa enzi zetu hizi ambapo wapo tusioheshimu ndoa. Tumefikia hatua ya kuziona kuwa kama mahusiano ya kawaida tu. Yafaa turudi tena nyuma na kuona utakatifu wake. Hapa ndipo tutajiletea baraka. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni