Jumatano, Agosti 11, 2021
Jumatano, Agosti 11 2021
Juma la 19 la Mwaka
Kumb 34:1-12
Zab 66:1-3, 5,8, 16-17(K) 20, 9;
Mt 18:15-20
UJASIRI WA KUPATANA
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza, tunasikia habari za kifo cha Musa. Musa anafariki bila kufika katika nchi ya ahadi. Yeye anaiona tu, anaioneshwa yote, lakini haruhusiwi hata kuikanyaga. Musa huyu ndiye aliyeteseka na umati wote wa Israeli, tangu kwenda kupambana na Farao, hadi anawaombea wana wa Israeli wapate mana na maji jangwani, akapigana vita mbalimbali, lakini mwisho wa siku hapati nafasi ya kuifurahia nchi ya ahadi.
Hapa ndugu zangu twajifunza mengi kuhusu maisha ya Mchamungu. Maisha ya Mchamungu ni kuandaa tu njia ili wengine wakafurahie. Maisha yetu ni sadaka. Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe alitambua hili hasa pale alipokubali kuutoa uhai wake kwa niaba ya mfungwa mwenzake.
Katika maisha ya wanadamu, wapo wanaofariki bila hata kuonja matunda ya kile walichopigania; wanaokuja kuonja ni wenzake. Somo hili litutie moyo hasa sisi ambao bado tunakazana na shughuli mbalimbali bila sisi wenyewe kufaidi. Tutiwe moyo na ukweli kwamba hata ikiwa sisi hatutafaidi matunda yetu, kizazi kijacho, au watoto wetu watayafaidi. Hivyo tuzidi kujitolea kwa ajili ya wenzetu.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anaeleza juu ya utume wetu na nafasi yetu katika kuwasahihisha na kuwaokoa ndugu zetu. Yafaa tuoneshe bidii kusahihishana na ndugu tuliokoseana nao. Yesu anasisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wenzetu katika kusahihishana na ndugu zetu. Hili ni jambo jema kwani machoni pa ndugu au mtu mwingine, hasa asiyeegemea upande wowote, ndipo tunapoweza kuona udhaifu wa kila mmoja wetu na kujitambua zaidi na kujirekebisha. Hivyo tutambue msaada wa wenzetu katika kusuluhisha madhaifu yetu katika jamii.
Tuwe pia na moyo wa kuwasikiliza wenzetu wanaotumwa kwa lengo la kurekebisha madhaifu yetu katika jamii. Tuepuke kiburi na majivuno na tuwapokee. Mwenye nia ya kusuluhisha madhaifu yetu katika jamii ni mpenzi wa Mungu. Hivyo tujitahdii sana kupokea ushauri toka kwao.
Maoni
Ingia utoe maoni