Jumanne, Agosti 10, 2021
Jumanne, Agosti 10 2021
Juma la 18 la Mwaka
Sikukuu ya Mtakatifu Laurent, Shemasi na Shahidi
2Kor 9: 6-10;
Zab 112: 1-2, 4, 9 (K) 5;
Yn 12: 24-26.
MBEGU YA AMANI
Karibuni sana ndugu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo tunapoadhimisha sherehe ya Mt. Laurent Shahidi. Huyu aliona fahari katika kutoa kwa ajili ya maskini, pale alipojitahidi kutoa na kuwatumikia maskini, alijikuta akibarikiwa na Bwana na kuongezewa mali iliyopaswa itumike kwa ajili ya maskini. Lakini viongozi na watawala wa serikali walimwonea wivu na kutaka kuchukua mali hizi. Hivyo waliishia kuchukua mali zake na mwishowe aliishia kufa kifo dini akiwatetea maskini wake aliowapenda sana.
Mungu alimkweza sana na kumpatia taji ya kuwa shahidi.
Masomo yetu leo yanatuongoza katika kutafakari vyema siku ya Mt. wa leo. Somo la kwanza linaelezea msisitizo wa Mt. Paulo akiwaambia wakristo wa Korintho juu ya utoaji. Anawaeleza kwamba kila mtu ajitahidi kutoa kadiri alivyojaliwa, kwa moyo wa upendo, bila manunguniko, kwani Mungu humpenda yeyote atoaye kwa ukarimu.
Haya ni maneno yaliyotumika kuwatia moyo wakristo wa Korinto ili watoe kwa ajili ya kanisa ya Yerusalem lililokuwa katika mateso makubwa na kutengwa na Wayahudi. Paulo anawakumbushia kuhusu faida iliyopo katika kutoa. Kutoa ni kwa ajili ya Bwana na hivyo Bwana humbariki yeyote atoaye kwa moyo wa ukarimu. Maneno haya yatutie moyo na sisi ili tuweze kutoa zaidi kwa ajili ya Bwana. Wengi wetu tunakatishwa tamaa pale tutoapo vitu ambavyo baadaye hutumika na wahudumu wa kanisa, wengi tunaona wivu na kusema kwamba tunatoa ili kuwatajirisha, hili sio kweli. Tuwe na imani ya kuona kwamba kile tutoacho ni kwa ajili ya Bwana.
Kingine ni kwamba katika utoaji, baadhi ya viongozi hawapaswi kuhubiri kila siku juu ya utoaji-watu wasilazimishwe kutoa. Wakristo waache watoe kwa ukarimu, kwa moyo mkunjufu. Siku hizi baadhi ya mahubiri ya viongozi wengi ni kutoa, kutoa. Sawa, lakini tuache kulazimishwa. Kila mtu na atende kadiri ya nafsi yake, akitambua ni wajibu wake kwa Mungu atoe kwa ukarimu na kwa imani kwa Mungu.
Katika somo la injili, Yesu anawaeleza wanafunzi wake juu ya ukuu uliopo katika kujitoa sadaka. Anasema ni pale tu tutakapokuwa tayari kujitoa sadaka, ndipo faida itakapoweza kuonekana. Sehemu inayokosekana watu wenye kujitolea, watu wenye kujitumikisha kwa ajili ya wengine-pale panapokosekana watu wa namna hii, hakika hapana maendeleo, pana wivu, pana matatizo makubwa, hakuna mwenye kufurahia sadaka ya mwingine. Familia haiwezi kusonga mbele ikiwa patakosekana mwenye kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine.
Hivyo tujitahidi sana tuwe watu wa kujitolea kwa ajili ya wenzetu. Popote tulipo tusiache kujitoa kwa ajili ya wenzetu. Hapa ndipo tutakapoweza kuzibariki jumuiya zetu na familia zetu. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni