Jumatatu, Agosti 09, 2021
Jumatatu, Agosti 9 2021
Juma la 19 la Mwaka
Kum 10ç 12-22;
Zab 147: 12-15, 19-20;
Mt 17:22-27
TUMECHAGULIWA KWA LENGO!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza, Musa anawaeleza wana wa Israeli wamche Bwana, anawaeleza wajitahidi sana kufanya hivi. Wajitahidi kupambana na aina yote ya matendo ambayo huwakwaza na kuwarudisha nyuma katika kumtumikia Bwana.
Na pia wanakumbushiwa kuwaheshimu wageni, wawapatie matunzo mazuri kwani hata wao waliwahi kuwa wageni katika nchi ya Misri.
Ujumbe huu unapaswa kutufikia na sisi pia ndugu zangu. Tuwakumbuke wageni pia. Wageni ni wale wasiojua mambo, wale wasiojua lugha fulani au wasiojua mambo yanavyokwenda katika maeneo fulani fulani. Mara nyingi tukikutana na watu kama hawa, tunatabia ya kusema kwamba hapa lazima tuwafaidi. Tupo tunaowauzia wageni bidhaa feki au kama mtu hajui kiingereza tunamtafsiria vitu tofauti. Tuwapende wenzetu wageni. Mwuzie kwa bei ile ile unayouzia watu wa kawaida, na mwuzie bidhaa bora. Pia kama ni kumtafsiria, tuwatafsirie vitu vya kweli. Hapa ndipo kumcha Mungu.
Katika injili, Yesu anajitahidi kulipa kodi. Hatafuti kisingizio bali anajitahidi na kulipa kila anachodaiwa. Nasi tusiache kulipa madeni yetu. Tujitahidi hadi senti ya mwisho. Kama unalo deni la mtu, jitahidi ulimalize lote. Usisingizie umaskini, au maisha magumu. Hakika tukubali kulipa hadi senti ya mwisho na Bwana atatubariki. Tuwe watu huru kabisa. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni