Ijumaa, Agosti 06, 2021
Ijumaa Agosti 6, 2021
Juma la 18 la Mwaka
Sikukuu ya Kung’ara Bwana wetu
Dan 7:9-10, 13-14;
Zab 96:1-2, 5-6, 9;
2 Pet 1:16-19;
Lk 9: 28-36
KUKAZA MACHO YETU KWA KRISTO NA UTUKUFU WAKE!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya kungara sura kwa Yesu. Ni sikukuu ambapo Yesu alingaa sura akionesha utukufu wake wa Kimungu kwa wanafunzi wake. Lengo lilikuwa ni kuwatia moyo kwamba wanachokifuata sio kitu cha uongo uongo bali wanamfuata Kristo aliye Mungu.
Ukweli ni kwamba kitendo cha Yesu kuwa wakawaida (simple) na kukaa na wanafunzi wake, kitendo cha yeye kutamani kuishi kwa muda mwingi kinyenyekevu kama mwanadamu, kulikuwa na hatari ya wanafunzi wake kumzoea mno na kushindwa kuuona ule Umungu wake. Mbaya zaidi kipindi hiki mateso na kifo chake yalikuwa ndio yanakariba na hivyo basi kama Yesu asingalikuwa amewaonesha tukio rasmi kudhihirisha Umungu wake, hakika wengi kati ya wanafunzi wake wangalirudi nyuma na kuacha kumfuata Yesu.
Leo Yesu katika injili anatangazwa na kudhihirishwa mbele ya wanafunzi wake wa tatu kwamba yeye ni mwana mpendevu wa Mungu na hivyo inabidi asikilizwe. Tukio hili kweli liliimarisha Imani za hawa mitume wa tatu kwani baada ya Yesu kufufuka kutoka wafu, kama tunavyoona katika somo la pili toka 2Petro 1:16-19, mitume kama Petro na baadaye Yohane walilitumia tukio hili kutangaza umungu na ukuu wa Yesu. Kweli hili halikuwa tukio la Yesu la kutamba mbele ya wanafunzi wake bali lilikuwa tukio la kuwatia moyo wanafunzi wake na kweli liliwatia moyo kweli.
Siku ya leo basi tunakumbushwa juu ya nguvu alizonazo Yesu wetu. Yeye ni mwana mpendevu wa Mungu. hivyo tumkimbilie leo, tumlilie, tumwambie Bwana sikiliza sala na mlio wetu leo sisi watoto dhaifu tusiokuwa na kitu. Tumwachie shida zetu. Duniani hatuwezi kubeba kila kitu peke yetu, na mbaya Zaidi yupo shetani anayefanya mambo kuwa magumu kila siku. Bila ya kumkimbilia Bwana hakika hatutafika popote. Hivyo siku ya leo basi tunaalikwa tumkimbilie Yesu; yeye anao Umungu wa pekee na hakika na kamwe hatatuacha. Nasi tusimuache leo bila ya kumweleza shida zetu.
Kingine ni kwamba tutambue kwamba Yesu alingaa sura lengo likiwa si kujitamba mbele za watu bali lengo likiwa ni kuimarisha imani yao na tukumbuke kwamba aliwachukua baadhi ya wanafunzi wachache ili kudhihirisha tukio hili na lengo basi ni ili imani yao ipate kuongezeka. Nasi ndugu zangu siku zote tubakie katika unyenyekevu kwani unyenyekevu ndio njia ya kwanza ya kutuokoa. Yesu alikuwa Mungu lakini hakuhangaika kujionesha. Basi na sisi hata kama tunao uwezo wa darasani au wa kipesa au wa kuongea sio wakati wa kuanza kujionesha nakutamba.
Wengi tunaanzaga kuwachukiza wengine na kuwafanya wengine wasifaidi karama hizo kwa sababu ya majivuno yetu na manyanyaso yetu. Wengi wameshindwa kusaidika na vipaji vyetu kwa sababu tumekosa unyenyekevu kama Yesu alivyokuwa nao. Tuwe wanyenyekevu na watu watafaidi vipaji vyetu. Karama au vipaji tulivyonavyo kamwe tusikubali viwe sababu ya watu kuanza kutuchukia.
Kingine ni kwamba tusikubali kumzoea Yesu hadi kufikia kumwona kama hana kitu kwani kuna tukio atatutendea ambalo litatufanya tuwe wapole kwake na kutunyenyekesha. Kamwe tusije tukamuona Yesu hasa kwenye sakramenti zake kana kwamba kaishiwa na hana jipya. Hii ni hatari sana. Tusikubali atumie nguvu zake kutunyenyekesha. Akiamua kukunyenyekesha kweli tutanyongonyea kweli. Tumheshimu na kumwabudu siku zote na kuepuka hali kama hizi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni