Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Julai 18, 2021

Kama Kondoo wasio na Mchungaji
Wakati Yesu na wanafunzi wake walipoenda mahali pa faragha kwa ajili ya kupumzika, makutano walienda mbio huko kumsikiliza na kupata Baraka. Makutano waliwaendea faraghani, lakini Kristo hakuwalaumu; waliingia bila kukaribishwa wala kutakiwa kwenye pumziko lao walilolistahili, lakini Yesu hakupatwa na uchungu wowote. Badala yake aliwaonea huruma akisema kwamba walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji. Ilikuwa ni umati wa watu, ambao walikuwa na hamu ya kufundishwa, lakini hapakuwa na mtu wa kuwafundisha; walihitaji kulishwa na mafundisho mazuri, lakini hapakuwa na wa kuwalisha. Kwa hiyo, Alikuwa na huruma juu yao, na hakuwafundisha tu, pia aliwaponya waliokuwa wagonjwa.

Katika somo la kwanza, Nabii Yeremia anaonesha kasoro za wachungaji wa taifa la Mungu. Kupitia Nabii Yeremia, Mungu anakemea tabia mbaya za viongozi wa Israeli zilizopelekea taifa zima la Mungu kuangamia kwa kupelekwa utumwani katika nchi ya Babeli. Mungu anaahidi kuchipusha chipukizi la haki kutoka shina la Daudi, atakayemiliki ufalme na kutenda kwa haki. Utabiri huu unatimia katika Yesu Kristo aliye mchungaji mwema wa kundi lake.

Yesu Kristo ni Mchungaji Mwema. Viongozi wa Agano la Kale walitambua na kujiona kuwa wamechaguliwa na Mungu kuliongoza taifa a Israeli, lakini walishindwa kutimiza wajibu wao ipasavyo. Kristo Yesu ni Mchungaji wa hakika. Alianza kuhubiri na kukusanya taifa la Mungu, amewagawia Mwili na Damu yake (Ekaristi Takatifu) na Neno lake, yaani mafundisho yake kwa watu wote.

Katika maisha yetu na katika sehemu mbalimbali kama vile: familia, jumuiya, serikali, kanisa n.k. viongozi na watu wanapaswa kuiga mfumo wa Yesu.

Tunakumbushwa tena leo wachungaji lazima wawe na upendo, huruma, upole, uvumilivu na unyenyekevu katika shughuli zao. Tukiwa tayari wafuasi wa Kristo tuwe na roho ya huruma kwa wenzetu.

Sala:
Bwana, tusaidie kuwa viongozi wema wenye kufuata mfano yako,
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni