Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Julai 20, 2021

Jumanne, Julai 20, 2021,
Juma la 16 la Mwaka wa Kanisa

Kut 14:21-15:1;
Zab 15: 8-10,12,17;
Mt 12: 46-50

MAPENZI YA MUNGU!

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Tafakari yetu ya neno la Mungu katika somo la kwanza tunasikia habari za wana wa Israeli kufanikiwa kuvuka katika bahari ya shamu. Kuvuka bahari ya shamu ilikuwa miongoni mwa matukio makuu yaliyoifanya Israeli ishangae, hadi imwimbie Bwana wimbo wa shukrani kwa sababu ya jinsi walivyouona ukuu na nguvu ya Mungu ikifanya kazi kati yao.
Katika kuvuka bahari hii, yapo makundi mawili ya watu. Wapo kwanza wamisri ambao walikuwa wanawakimbiza wana wa Israeli na wapo pia wana wa Israeli waliokuwa wametoka utumwani Misri. Wote wanaingia katika bahari moja baada ya maji kugawanyika. Cha ajabu ni kwamba baada ya muda sio mrefu, mgawanyiko unatokea. Maji yalirudi na cha ajabu, yale maji yakaleta utengano, yaliwauwa wale Wamisri, wale ambao hawakushiriki katika kumla mwanakondoo na kuwaacha waisraeli, wale ambao walishiriki katika kumla yule mwanakondoo.
Hivyo nguvu ya damu ya Mwanakondoo ilikuwa ikifanya kazi ndani yao. Tukio hili linaashiria pia maisha yajayo-kwamba kwa nguvu ya sakramenti tuzipewazo za kanisa, hakika tutaweza kuvuka na kufikia mbinguni. Wamisri walikosa kinga ya yule mwanakondoo na ndio maana walikufa maji. Wana wa Israeli walikuwa na nguvu, kinga ya yule mwanakondoo, damu yake ilikuwa bado na nguvu ya kuwalinda na ndio maana hawakuweza kufa maji. Sisi tuzidi kuziheshimu sakramenti hizi. Zitatuwezesha kuvuka na kufikia upande wa pili wa bahari yaaani mbinguni.

Katika somo la injili, Yesu anamtangaza yeyote yule anayetii mahusia yake ndiye baba na mama yake. Kwa kusema hivi, Yesu anajitangaza kuwa rafiki na ndugu wa yeyote. Hivyo kuyashika maagizo ya Yesu ni jambo la muhimu. Hili linatutangaza, linatutambulisha kuwa kaka na dada wa Yesu. Kuwa kaka na dada wa Yesu ni thamani kubwa.
Hii ni ashirio la uwepo wa uhusiano mkuu, uhusiano wenye kutuletea mema. Hivyo tutambue kwamba matendo mema huimarisha uhusiano wetu na Mwenyezi Mungu. Hili litutie moyo katika kutenda matendo mema. Kila jema tulitendalo ni hazina kwetu kwani hakuna kinachopotea. Wema hauozi, kama huoni faida yake kwa sasa, utaipata baadaye. Tusiache kutenda mema. Mema yetu yatatutetea. Bwana unisaidie nipate moyo wa kutenda mema.

Tumsifu Yesu Kristo...

Maoni


Ingia utoe maoni