Jumamosi, Julai 17, 2021
Jumamosi, 17 Julai, 2021
Juma la 15 la Mwaka
Kut 12:37-41
Zab 136:1-10
Mt: 12:14-21
Usiku Mtakatifu Sana.
Wana wa Israeli wanakumbushwa katika somo la kwanza kuuheshimu usiku ule mtakatifu, walipoondoka nchini Misri, pale walipomla mwana kondoo na kuokolewa na Mwenyezi Mungu wasilipate lile pigo la kumi lililowaacha Wamisri mahame. Wanaambiwa wasiache kuadhimisha tukio hili kizazi baada ya kizazi.
Katika usiku huu, waliiona nguvu ya Bwana, waliona hekima yake na uaminifu wake na upendo wake kwao. Hivyo, lazima wauadhimishe kama fundisho kwa vizazi vijavyo, na pia kama sehemu ya wao kushiriki neema za Mwenyezi Mungu, neema zilizotolewa katika usiku huu na kumuomba azidi kuwabariki. Yesu alipokuja, jioni kabla ya kuteswa kwake, alishiriki katika kuadhimisha usiku huu mtakatifu. Lakini ndani ya huu usiku, hakumchinja mwanakondoo kama ilivyokuwa desturi bali alitegemea yeye mwenyewe kutolewa kama mwanakondoo asiye na doa. Halafu, alichukua mkate, akaubariki na kikombe vile vile kilichojaa divai akabariki akasema huu ni mwili wangu, na hii ni damu yangu-na kutoa amri kwa sadaka hii na tendo hili kuendelezwa kwa vizazi vyote hadi ile siku atakayokuja. Kwa waisraeli, ilikuwa ni kosa kubwa kuacha kuiadhimisha pasaka, kama ilivyo na sasa kwetu, ni kosa kubwa kuacha kuiadhimisha pasaka kwani ni kukosa 'appreciation' ya sadaka iliyotolewa na Baba na pia vizazi vijavyo vitashindwa kujifunza.
Sisi tupende kuadhimisha pasaka yetu. Hakika ni tendo takatifu kuadhimisha pasaka hii. Pia yafaa tusiache kuadhimisha sikukuu mbalimbali kama birthdays, anniversary ya ndoa, upadre yote haya kila tunapoadhimisha, ni namna ya kukiri wema na uwezo mkuu wa Mwenyezi Mungu ndani ya maisha yetu na kumwomba azidi kutubariki. Sisi tusiache kuadhimisha kumbukumbu mbalimbali katika maisha yetu. Zinaonesha kuthamini kile alichokupa Mungu.
Katika somo la injili, Yesu anaamua kuondoka baada ya chuki dhidi yake kuongezeka na mipango dhidi ya kumteketeza inavyozidi. Yesu haondoki sio kwa sababu ameogopa bali kwa sababu hapendelei fujo na kundi fulani au ugomvi. Ndivyo Yesu alivyo. Lengo lake halikuwa kuleta fujo. Na alipoona kwamba kuna kikundi fulani cha wataka fujo, aliamua kuwakwepa lengo likiwa ni kuleta amani.
Sisi tuige tabia ya Yesu. Tusiwe wachochezi ndugu zangu bali tuwe watu wenye kutoa msaada na kutafuta amani ndani ya maisha yetu na dunia nzima. Tusichonganishe ndugu na kuwaona wanagombana nasi tunachekelea kwa mbali. Tuwe waleta amani na wapatanishi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni