Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Julai 14, 2021

Jumatano, Julai 14, 2021.
Juma la 15 la Mwaka

Kut 3:1-6, 9-12;
Zab 103:1-4, 6-7;
Mt 11:25-27


SIRI YA UFALME WA MUNGU ILIYO FUNULIWA KWA WATOTO!

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari ya neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na Mungu akimtokea Musa katikati ya kichaka kilichowaka Moto lakini hakikuungua. Inaelezwa na Wanatheologia kwamba Musa alikuwa katika sala na maombi mazito juu ya watu wake huko Misri alipokuwa Midiani.
Tangu amkimbie Farao na kwenda katika nchi ya Midiani, yeye aliendelea kusali na alipokuwa katika mawazo mazito haya, muujiza huu ulimtokea. Kwa kawaida, moto una tabia ya kuharibu kila kitu. Hata maono yamhusuyo Mungu, macho yake yanatangazwa kama macho ya moto, macho yenye uwezo wa kuona chochote, hakuna kiwezacho kufichika mbele ya macho yake.
Lakini cha ajabu leo kichaka kinawaka moto, bila kuteketea. Ni ishara ya Mwenyezi Mungu anayeteseka na watu wake huko Misri, lakini watu hao hawatateketea, bali watapata wokovu. Ukitafakari juu ya muujiza huu, kwamba uliwezekanaje, basi tutapata imani juu ya mambo mengi, na dogma nyingi zihusuzo kanisa.
Kwanza, ni juu ya ubinadamu na Umungu wa Yesu. Yesu ana hali ya Umungu na ubinadamu kwa wakati mmoja. Umungu wake ni kamili na ubinadamu wake ni kamili pia. Hali hizi zote zipo katika Yesu, ndani ya nafsi moja katika muungano maalumu lakini bila kuchanganyikana. Bikira Maria alimzaa mtoto Yesu bila kupoteza ubikira wake. Kama kichaka kiliweza kuwaka moto bila kuteketea, ndivyo inavyowezekana kwa asili tofauti kukaa pamoja bila kuchanganyikana. Haya ndiyo maajabu ya Mungu.
Tendo la Kichaka kuwaka moto bila kuteketea litutie moyo na sisi tuweze kuwa na imani kuhusu dogmas za kanisa.
Katika injili ya leo, Yesu anashangilia kwa Mungu kuwafunulia ukuu wake watoto wachanga. Watoto wachanga yamaanisha watu wanyenyekevu, wenye kusikiliza. Bwana huwapenda watu wenye kusikiliza. Hata kwenye kuwachagua wa kupewa habari za kuzaliwa kwa mwanae, aliwachagua wachungaji, wao walikuwa na moyo wa kinyenyekevu. Hawa ndio waliotegemewa kumsikiliza.
Angewachagua labda wafanyabiashara, hakika habari zisingepokelewa kwani wafanyabiashara ni watu wanaopinga chochote kile kinachowasabishia hasara. Hawapo tayari kupoteza muda kwa mambo yaliyokinyume cha biashara zao. Hata kwenye kuwachagua wanafunzi, alichagua watu wa chini. Kwa sababu hawa ndio wenye utayari wa kukaa na mtu kwa masaa mengi wakimsikiliza. Mungu awapenda wanaosikiliza, wanaotenga muda wao kuongea naye. Sisi tutambue kwamba tukimsikiliza Mungu ndivyo tutakavyoweza kufaidi. Wengi wetu tumeachwa, na tupo katika hali ya shida zaidi kutokana na ukosefu wa usikivu. Tuwe watu wasikivu, wenye kusikiliza wengine. Tumsifu Yesu Kristo.

Sala:
Bwana, ninakuja tena kwako kwa kukuamini. Nisaidie mimi nitambue kuwa hekima yote inatoka kwako Baba na sio kwangu. Nisaidie mimi nikugeukie wewe daima kama mtoto na nisaidie maisha yangu yabaki ya kawaida kama unavyo tamani. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni