Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Julai 06, 2016

Jumatano, Julai, 6, 2016,
Juma la 14 la Mwaka wa Kanisa

Hos 10: 1-3, 7-8, 12;
Zab 104: 2-7;
Mt 10: 1-7

KUWA MMISIONARI!

Injili ya leo inaonyesha maelekezo kwa wafuasi wa Yesu jinsi ya kufanya kazi yao ya umisionari na mambo yanayoweza kuwapata. Inaanza kwanza na kuitwa kwa wafuasi kumi na mbili ambao hawa wanaitwa Mitume. Mfuasi (kwa kilatini discipulus- maana yake “kujifunza”) ni mtu anayefuata mwalimu ili kujifunza na kuweka mafundisho ya mwalimu wake katika maisha yake. Mtume (kwa Kigiriki Apostolos) ni yule anayetumwa kwa kazi ya kutangaza mafundisho ya mwalimu wake.

Tunaitwa kuwa wafuasi na tunatarajiwa kuwa mitume, kwa moyo wote tuweze kuwashirikisha wengine Imani yetu. Ni rahisi kujiona wenyewe kama Wakatoliki wa ‘kawaida’, kama wafuasi tu, na kuwaona Mapadre na Watawa kama wao tu ndio wafanya kazi wa utume wa Kanisa. Hii itakuwa sio sahihi. Sisi wote tumeitwa kuwa wafuasi kwa njia ya ubatizo wetu na Kipaimara, pia tumeitwa kuwa mitume.

Sisi tupo wapi katika kufanya utume wetu? Je, tuna ujasiri ndani yetu ili tuweze kufika sehemu za giza kabisa ambapo neno la Yesu halijafika bado? Au sisi ni dhaifu ndani yetu kiasi cha kushindwa hata kumshuhudia Yesu katika maeneo yetu tunayoishi? Yesu anawataka wamisionari wanaojitoa sio watu maalumu bali wafuasi wake wote wanaofanya mapenzi ya Baba yake.

Sala: Bwana Yesu Kristo, umetuita sisi ili tutangaze Injili yako ya Matumaini na ukombozi hapa katika maeneo yetu na ulimwenguni kote. Tufundishe kuwa wamisionari waaminifu kwa maneno na matendo. Amina .

Maoni


Ingia utoe maoni