Alhamisi, Julai 08, 2021
Alhamisi, Julai 8, 2021,
Juma la 14 la Mwaka
Mwa 44:18-21, 23-29; 45:1-5;
Zab 104:16-21;
Mt 10:7-15
KUPEWA NGUVU NA INJILI
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu ya neno la Bwana katika somo la kwanza Yusufu anaonesha moyo wa huruma na masikitiko kwa wenzao. Nao ndugu zake ambao hapo awali walimuuza Misri nao wanapatwa na aibu kubwa na mshtuko kwamba waliyetegemea kwamba wamemwangamiza, kumbe kwa sasa ametokea mbele yao kama mkuu, mwenye mamlaka makubwa mbele yao ambao kwa sasa hawawezi tena kuyashinda.
Wakati akiwa mdogo, kaka zake walikuwa na umbo na umri mkubwa na hivyo walitumia nguvu zao kumfanyia ukatili. Lakini sasa Yusufu amekwishakuwa mkubwa na ni mwenye mamlaka makubwa; analo pia na jeshi kubwa ambalo kwa sasa hawawezi kumshinda. Hakika ndugu zake walipata mshtuko mkubwa.
Huu ni mwaliko kwetu kwamba tuwaheshimu wote. Hata wadogo tulio nao tuwatunze vyema. Tusiwadhulumu kipindi hiki walipo wadogo na dhaifu. Muda sio mrefu nao watapata nguvu pia. Tusitumie miili yetu mikubwa kuwanyanyasa au kuwatendea uovu wowote. Yusufu anakataa kuonesha moyo wa kisasi kwa nduguze. Alitambua kwamba Mwenyezi Mungu ameamua kufanya haya akiwa na lengo maalumu. Hivyo aliweka imani mbele kuliko visasi. Hili lilimfanya azidi kubarikwa zaidi.
Nasi tutambue kwamba tutabarikiwa kwa kuepuka visasi. Wale tuliowahi kunyanyaswa halafu baadaye tukafanikiwa-tutambue kwamba tutapata mafanikio zaidi pale tutakapoweza kuondoa visasi na kuweka imani mbele kuliko chuki. Tusikubali kuzima baraka zetu kwa njia ya visasi.
Katika somo la injili, Yesu anatoa maagizo kwa wanafunzi wake namna ya kuihubiri injili. Katika kuihubiri injiili, anasisitiza kwamba waweke injili mstari wa mbele kuliko yote. Wamtegemee Mungu, wasikubali kulimbikiza ya dunia. Kazi ya Bwana ni rahisi kusahauliwa kirahisi au kufunikwa na mambo ya dunia. Hivyo yafaa mambo ya Mungu yapewe kipaumbele. Hatari hii ndio tunayoiona hadi nyakati zetu. Kazi ya Bwana haipewi kipaumbele. Mambo ya dunia yanaifunika injili. Hata sisi tupo tayari kukosa kanisani, au kupunguza muda wa sala ili tupate kufanya biashara au harambee fulani. Hatupaswi kufunika mambo ya Mungu kwa malimwengu. Malimwengu ni hatari kwa uenezi wa injili ya Bwana.
Maoni
Ingia utoe maoni