Ijumaa, Julai 09, 2021
Ijumaa, Julai 9, 2021,
Juma la 14 la Mwaka
Mwa 46:1-7, 28-30;
Zab 36:3-4, 18-19, 27-28, 39-40;
Mt 10: 16-23
KONDOO NA MBWA MWITU!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika tafakari yetu ya neno la Bwana, katika zaburi yetu ya wimbo wa katikati, tunakutana na maneno yasemayo kwamba wokovu wa wenye haki u na Bwana. Maneno haya ya zaburi yanatumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza ambapo Yakobo na familia yake yote inapata kuokolewa kutoka katika njaa iliyokuwa inalikabili taifa la Kanaani. Analetwa Misri na kuufanya uhai wake uokoke; yeye na familia yake. Hakika wokovu wa wenye haki u na Bwana kwani tukijaribu kuangalia namna jinsi huu wokovu ulivyoletwa, hadi Yakobo na uzao wake unakuja kuokolewa na njaa hakika inashangaza.
Hapa ndio tunapoweza kuona mkono wa Mungu katika tukio hili. Kumbe tukio tulilolidhania kwamba ni la kikatili, limegeuka kuwa tukio la kuleta neema kwa familia nzima. Hakika Mungu ana mipango mingi ajabu. Yeye aweza hata kugeuza ugumu wetu kuwa furaha. Hivyo tusilalamike sana kwa wale ambao tumewahi kutendewa ukatili na wenzetu, usilalamike. Ni kumwomba Mungu alete mema ndani ya huo unyama uliokwishatendewa kama ilivyotokea kwa Yusufu.
Usibakie katika kulalamika na kukata tamaa. Tambua kwamba Mwenyezi Mungu aweza kubadili ubaya uliotendewa kuwa uzuri wenye kuleta furaha ya ajabu.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anawaeleza wanafunzi wake waziwazi kwamba wajihadhari na wanadamu. Wanadamu wanaelezwa kama kikwazo chao cha kwanza kwao. Hawa ndio watakaowapeleka katika masinagogi na kuwafanya wachapwe viboko. Lakini wanatiwa moyo na Yesu leo. Wanaagizwa kwamba wakifukuzwa katika mji huu, waende mji mwingine. Wasikate tamaa kwa kufukuzwa katika eneo moja. Haimaanishi kwamba watakataliwa na wote, wapo watakaowapokea.
Hili liwe fundisho kwetu ndugu zangu. Tukikataliwa katika eneo mojawapo au ukikatishwa tamaa na mtu mmojwapo, jaribu pia mwingine. Haimaanishi kwamba wewe utakataliwa na wote. Hili litutie matumaini hasa katika kuihubiri injili. Injili imerudi nyuma kwani watu tunakatishwa tamaa kirahisi mno. Hatuna utayari wa kusema kwamba tukikataliwa eneo moja, twende jingine. Wapo tunaofikiri kwamba ukikataliwa na mmoja basi kwa wengine itakuwa hivyo hivyo. Hii ni mbinu shetani anayotumia kuirudisha nyuma injili au kutufanya tushindwe kufanya maridhiano ndani ya jumuiya zetu. Hivyo njia moja ikishindwa, jaribu nyingine. Kwa namna hiyo utafanikiwa kuleta maridhiano katika jamii, utaweza kutatua mengi ndani ya jamii na kufanya pia injili isonge mbele. Ukichukiwa na mtu mmoja usidhani dunia yote inakuchukia. Wapo wanaokupenda.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni