Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Julai 06, 2021

Jumanne, Julai 6, 2021,
Juma la 14 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mt. Benedikto, Abati

Mwa 32:23-33;
Zab 16:1-3, 6-8;
Mt 9:32-37


KUSIMAMA IMARA KATIKATI YAVIPINGAMIZI!
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na Yakobo akiendelea kuneemesha maisha yake na kuyapatia baraka. Leo katika masomo yetu anaonekana kuwa mtu wa bidii aliyekuwa na uchu wa kubarikiwa. Aliogopa sana laana maishani mwake. Kila aliyekutana naye alijitahidi kuomba baraka.
Alipendezwa kuwa na sifa nzuri na baraka maishani. Na leo Mwenyezi Mungu anabadili jina lake toka Yakobo kwenda Israeli kumaanisha kwamba hakika amekuwa kiumbe kipya cha Bwana chenye kubarikiwa naye na kupokea wingi wa neema zake. Nasi tuwe watu wa kuomba baraka za Mwenyezi Mungu maishani. Tunaokaa nao tuishi nao vyema ili tupate baraka toka kwao. Kama ni wagonjwa tunawatunza, tuwatunze kwa roho nzuri ili tuchote toka kwao baraka. Kama ni wafungwa, wazee, yafaa tuwatunze vyema na kuchota kwao baraka; tuwabembeleze tupate toka kwao baraka na sio laana. Maisha ya wengi wetu imejaa mikosi na shida kwa sababu ya kushindwa kubembeleza baraka toka kwa wenzetu. Tusikubali vinywa vyetu viwe sababu ya sisi kulaaniwa.
Katika somo la injili, baadhi ya Wafarisayo wanamkejeli Yesu kwamba anatoa pepo kwa nguvu ya Mkuu wa pepo. Wivu wa Wafarisayo uliwafanya washindwe kuelewa juu ya ukuu wa nguvu ya Mungu. Mwishowe wakaona kwamba shetani ni mwenye nguvu kuliko Mungu. Ndivyo wivu ulivyombaya ndugu zangu. Wivu hutufanya tuone kwamba shetani ni Mwenye nguvu sana na kila mahali anafanya kazi kuu. Lakini tunashindwa kuona nguvu ya Mwenyezi Mungu maishani mwetu na maishani mwa maisha ya wengine. Hii ndio hasara ya wivu. Mwenzetu akifanikiwa, wivu utatutuma kusema kwamba ni Freemason na kushindwa kuona kwamba Mungu aweza kufanya kazi ndani ya maisha yake pia. Hivyo tujue kwamba wivu wetu ndio utakaompatia shetani mamlaka.
Dunia bado inahitaji watu wanaopaswa kuwaelimisha wengine hasara za mambo haya. Tuache kukumbatia vitabia hivi vya wivu. Hakika ni vitabia hatari sana kwa maisha yetu. Tumwombe Bwana atume wafanyakazi wengi katika shamba lake ili watusaidie katika kutuelewesha hasara za mambo haya.

Maoni


Ingia utoe maoni