Jumanne, Juni 29, 2021
Jumanne, Juni, 29, 2021,
Juma la 12 la mwaka wa Kanisa.
Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume
Mdo 12:1-11;
Zab 33:2-9;
2Tim 4:6-8, 17-18;
Mt 16:13-19
MATESO YETU YA KILA SIKU YANATUSAIDIA KUKUWA KATIKA UHUSIANO NA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwenye tafakari ya neno la Mungu siku ya leo tunapoadhimisha sherehe ya watakatifu Petro na Paulo. Hii ni miamba mikubwa ya kanisa iliyolisaidia sana Kanisa. Walitumia muda, akili na uhai wao kwa ajili ya Kristo. Kwao, kuishi ilikuwa ni Kristo na hata kufa ilikuwa ni faida. Na hili walilidhirisha kwenye maisha yao. Kweli walikuwa watu wa imani na Mungu aliwasaidia sana kwenye utume wao huu kwa kanisa na hili linadhihirishwa katika masomo yetu ya leo.
Katika zaburi ya wimbo wetu wa katikati leo, tunakutana na mzaburi anasali akionesha Imani kubwa kwa Mungu kwamba kamwe hataacha kumtukuza na kumheshimu Bwana na anawaalika watu wamtukuze Bwana pamoja naye kwani Bwana amekuwa mwema kwake kila wakati kwani aliwahi hata kumtuma malaika wake akamuokoa kwenye hatari na kumfanya asiabike mbele ya maadui wake. Jambo hili linamfanya asiache kuyatangaza matendo makuu ya Mungu na anaahidi kwamba kamwe hataacha kuzitamka sifa za huyu mwenyezi Mungu kwa msaada wake huu.
Kwenye masomo yetu ya leo, miongoni mwa watu waliokutana na msaada kama huu ni Petro mtume ambaye kwenye somo la kwanza, habari hii inaelezewa, jinsi Mungu alivyomuokoa mikononi mwa adui katili kabisa-Herode, aliyetaka kumnyonga mbele ya watu. Petro alimshukuru Mungu sana kwa hili tukio na alitambua kwamba ni malaika wa Bwana ametumwa ili kumwokoa. Mtume Paulo naye aliokolewa kwenye matukio makubwa na malaika. Yeye alipotaka kuuawa kule mjini Dameski, alitelemshwa nje ya mji kupitia kapu. Hapa napo ni malaika tu aliyetumwa ili kumwokoa.
Ndugu zangu, mitume hawa walipewa ulinzi wa hali ya juu na Mungu kwani pia walikuwa mihimili mikubwa kwa kanisa. Yesu asingaliruhusu wafe kabla ya wao kutimiza ule utume wao na waliache kanisa kwenye hali nzuri. Wao walijitoa mno kwa ajili ya Mungu na Mungu alijitoa kwa ajili ya kuwalinda. Nasi ndugu zangu tusiache kujitoa kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kama sisi ni mapadre, masista, makatekista, watawa, waamini tujitoe kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kazi yake tuiweke mstari wa mbele. Kama ni padre-tutambue kwamba utume kwa ajili ya watu wa Mungu ndio cha kwanza-fanya hivi naye Mungu atatubariki. Tukijidai kuhangaikia maslahi nakueleza hatutavuna chochote. Kwa mwanzoni tutafikiria labda tunavuna pesa lakini baadaye kumbe tutajiona kwamba kweli hatujafanikiwa kwenye chochote. Hata zile mali ulizojidai kutumia muda wote kuzianzisha itafika mahali ziishe kama hewa-au mtu atakudhulumu na utaishia kujiona kana kwamba kazi zako zote ni bure. Wote walioacha kazi ya Bwana na kuishia kwenye kujitafutia maslahi, wameishia tu kuanzisha vitu vilivyokuja kuishia kwenye kudhulumiwa na wenzao. Hivyo jamani tuithamini kazi ya Bwana. Tuiweke iwe mbele kabisa. Kazi ya Bwana itakutunza tu, itakufanya upate ulinzi kama Petro na Paulo walivyopatiwa. Mungu atatuepusha na magonjwa mbalimbali na ajali za namna mbalimbali kwasababu sisi ni watumishi wake na tunaithamini kazi yake. Hivyo, Mungu atakupatia ulinzi na upendeleo wa pekee. Fanya hivi ndugu yangu na kweli tutatambua ukweli wa jambo hili. Awe padre, awe katekista, sista, mwenyekiti jumuiya-wewe fanya hivi, ipe kazi ya Bwana nafasi ya kwanza kama haitakutunza. Wewe fanya hivi na hakika utaona tu. Mimi nasema kile nilichowahi kukiona maishani.
Katika somo la injili, tunakutana na Petro akimkiri kwamba Yesu ni Masiha. Petro alikuwa wa kwanza miongoni mwa mitume kutambua hili kwa hekima na uwezo wa hali ya juu sana. Paulo naye alilionyesha hili kwamba anamkiri Yesu kama Masiha katika nyaraka zake mbalimbali. Nasi kama Petro na Paulo tumkiri Yesu wetu kama Masiha. Hakika atatulinda tu na kamwe hatatuacha. Tumkiri huyu Yesu, tusimuache, jitoe kwa ajili ya Yesu naye atajitoa kwa ajili yako. Ukijitoa kwa ajili yake atakulinda tu hata kuacha. Atakuokoa. Hawezi kukuacha bila ulinzi. Tafakari hii jamani iwafikie wakristo wote-na tujitoe zaidi kwa kazi ya Kanisa tukisukumwa na tafakari hii. Tukiambiwa kwamba kuna kazi ya kupamba kanisani au kudeki kanisani, tuwe wa kwanza kukimbilia-pale ndio penye neema jamani. Tusiache hivi.
Maoni
Ingia utoe maoni