Jumatatu, Juni 28, 2021
Jumatatu, Juni 28, 2021,
Juma la 13 la Mwaka wa Kanisa
Mwa. 18:16-33;
Zab. 103:1-4, 8-11 (K) 8
Mt 8: 18-22
MFUASI, HAPA NA SASA!
Karibuni sana Ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika tafakari ya neno la Bwana asubuhi hii, katika Zaburi yetu ya wimbo wa katikati, tunakutana na ujumbe usemao: Bwana amejaa huruma na neema. Haya ni maneno ya ushuhuda ya Daudi kuhusu wema wa Bwana.
Na leo yanatumika kusisitizia jinsi huruma iliyokuu juu ya watu wa dunia kwa kuonesha jinsi alivyokuwa tayari kuwapigania watu wa Sodoma na Gomorah. Anakubali kusema kwamba kama kuna watu kumi ndani ya Sodoma, hakika hatakubali kuuharibu ule mji. Hakika Bwana amejaa huruma, uwepo wa watu wachache wenye haki kumi aweza kuufanya mji wote uokoke. Hakika Mungu anaangalia mema zaidi kuliko mabaya. Kati ya mji wenye maelfu, yeye akiona wema wa watu kumi, hakika atauokoa mji huo. Basi tujitahidi kuwa wenye haki. Usichoke kutenda mema. Wema wako utaiokoa dunia. Sodoma ingeokolewa kwa uwepo wa watu kumi. Sisi tusiache kujitahidi katika kutenda mema. Mungu akisimama na kumuona Mtu kama Mt. Fransisko mmoja katika mji, hakika hasira yake hubadilika.
Sisi tujitahidi kutenda mema. Tujue kwamba wema wa mtu mmoja utawaokoa maelfu. Tuwe watu wa kujitoa sadaka zaidi, na tusichoke kutenda mema. Watajitokeza watu mbalimbali kutupinga au kutukatisha tamaa lakini tutambue kwamba wema wako utaiokoa dunia. Usiache kutenda wema ndugu yangu.
Katika somo la injili, yupo Mwandishi anayetangaza kumfuata Yesu. Yesu anatoa jibu kwamba Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana vioto, lakini mwana wa adamu hana pa kukilaza kichwa chake. Yesu alitoa jibu hili sio kwamba alitaka kumzuia huyu mwandishi aache kumfuata bali alitaka ajue maana halisi ya kumfuata Yesu.
Huenda huyu mwandishi alifikiri kwamba kumfuata Yesu ni kuwa maarufu zaidi, ni kuwa tajiri na mtu mkubwa zaidi na kupata cheo kikubwa katika serikali yake ya kimasiha. Hivyo alihitaji afundishwe, ajue kwamba kumfuata Yesu ni kuubeba msalaba pia na sio umaarufu na ikiwa angefanikiwa kurekebisha hili, basi angekuwa mtumishi bora. Nasi tunaalikwa kurekebisha madhaifu yetu. Huenda kwenye kumfuata, tulianza na malengo tofauti, na hatukuelewa vyema maana ya wito wetu. Tunaalikwa leo kuyarekebisha na hivyo tutakuwa vyema.
Na mtu wa pili katika injili ya leo, anakaribishwa amfuate Yesu. Yesu anamuona kwamba anafaa na anaelewa maana ya kumfuata na atakuwa tayari kutoa sadaka. Lakini yeye anaona kana kwamba kumfuata Yesu kuna sadaka kubwa sana. Na ndio maana anataka aende nyumbani kwanza, anataka asubiri ili ale kwanza raha za dunia, ili akamilishe mambo yake halafu ndio amfuate. Yesu anamwambia kwamba aanze kumfuata sasa. Asisubiri kesho. Sisi tumfuate Yesu leo.
Maoni
Ingia utoe maoni