Ijumaa, Juni 25, 2021
Ijumaa, Juni 25, 21
Juma la 12 la Mwaka
Mwa 17: 1, 9-10, 15-22;
Zab 128: 1-5;
Mt 8: 1-4
KUWA KAMA KRISTO KATIKA KUPENDA NA HURUMA
Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, moyo wenye upendo mkubwa.
Injili ya Yohane inatuambia kwamba Moyo huu ulitobolewa; na ulipotobolewa, palitoka damu na maji (Yn 19:34). Maji ni ishara ya utakaso na damu ni ishara ya upatanisho. Maji na damu ni ishara ya sakramenti mbalimbali ambazo hububujika ndani ya mwili wa Yesu kutupatia utakaso na kutupatanisha na Baba.
Moyo huu umetupatia sakramenti mbalimbali ambazo kwazo twaweza kupata utakaso na kupatanishwa na Baba. Leo tujifunze kuzitumia sakramenti zetu vyema.
Katika masomo yetu leo, tunaelekezwa kutafakari kuhusu Mchungaji Mwema. Katika somo la kwanza, Mwenyezi Mungu anajitambulisha yeye kuwa mchungaji mwema, yeye anaahidi kuwaganga wenye majeraha, kuwalisha malisho salama na kuwaokoa mikononi mwa wote waliotaka kuwadhuru. Wafalme wa Israeli walishindwa kulilisha kundi la Bwana. Waliwaongoza katika kuabuu sanamu, dhuluma na katika kutenda uasherati. Hivyo kundi lote likaishia kula jalalani na kushindwa kuboresha maisha yao. Mwenyezi Mungu anaamua kulilisha kundi lake.
Katika injili leo, Yesu anajidhihirisha kwamba Yeye ndiye mchungaji wa kweli aliyetumwa ili kuhakikisha kwamba wote hawapotei. Anatangaza kwamba hata mmoja akipotea, atakuwa tayari kumtafuta. Sisi tukubali kuwa kondoo kweli. Nyakati zetu, changamoto tunazokumbana nazo ni changamoto ya kondoo kuwa wakaidi na kukakataa mwongozo wa mchungaji.
Kondoo wanajiamulia wenyewe juu ya nini wanachotaka kuamini. Hivyo wanaishia tu kufanya mambo ya hivihivi na kujichagulia malisho na kuishia kula jalalani.
Pia changamoto nyingine ni ya wachungaji wakorofi, wakatili na wenye kuwatesa kondoo. Na pale wanapokuwa kati ya kondoo, wanakuwa kweli mbwa mwitu. Kondoo wanakimbia. Haya ni mambo tunayopaswa kubadilisha. Tunapaswa kuwa wachungaji wema kweli. Tuache kuwaonea kondoo kweli. Sikuukuu hii ya moyo wa Yesu inatualika kuwa wachungaji wema. Yesu aliutoa uhai wake kwa ajili ya wengine. Wachungaji wawe watu wa kujitolea, wenye kuridhika na kile wanachopata, wajue kwamba kazi ya Bwana ni kujitolea; usitegemee kwamba kila kazi utakayopewa na Bwana utapokea mshahara. Na kondoo wawe wasikivu, wenye kufuata mwongozo wa wachungaji kwani siku hizi kondoo wengi nyakati hizi wanakula jalalani; hii ndio shida yetu.
Moyo mtakatifu wa Yesu utusaidie sisi kondoo kufungua macho na kuona chakula bora kinachopatikana katika Yesu na hivyo kukazana kupata chakula hicho. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni