Alhamisi, Juni 24, 2021
Alhamisi, Juni, 24, 2021,
Juma la 12 la mwaka wa Kanisa
Sherehe ya kuzaliwa kwa Mt.Yohane Mbatizaji
Is 49: 1-6;
Zab 138: 1-3, 13-15;
Mdo13: 22-26;
Lk 1: 57-66, 80
ISHARA YA UTUKUFU YA JUA LA HAKI !
Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sherehe ya kuzaliwa Mt. Yohane Mbatizaji. Kanisa lina kila sababu ya kuadhimisha kuzaliwa kwake kwa sababu kuzaliwa huku kulifungua ukurasa mpya kwa ulimwengu.
Yeye ndiye aliyemtambulisha Masiha kwa ulimwengu. Ndiye pia aliyeiandaa mioyo ya watu ipate kutubu ili Masiha aweze kuingia ndani ya mioyo hiyo. Yohane alikuwa mtu wa kujitolea, alijitolea sana kusaidia utawala wa Kristo kuenea ulimwenguni. Na yeye ndiye aliyeandaa mazingira yote.
Tunaalikwa leo kumwiga Yohane Mbatizaji. Tuwe watu wa kutubu dhambi zetu ili Kristo apate kuingia ndani ya mioyo yetu. Pia tukubali kusaidia katika kueneza utawala wa Kristo kwa akili na rasilimali zetu. Tusitumie vipaji vyetu kukuza utawala wa shetani. Wapo wasanii na wanasayansi wenye kutumia akili zao kumpinga Mungu.
Katika somo la kwanza, tunasikia habari za mtumishi wa Mungu, aliyechaguliwa tangu tumboni mwa mama yake ili kutangaza wokovu kwa mataifa na kuziinua kabila za Israeli zilizoanguka. Mtumishi huyu alichaguliwa na Bwana na alikubali kutii sauti ya Bwana na kuitika kuwa mtumishi wake na kusaidia katika kuitenda kazi ya Bwana. Yohane Mbatizaji alikuwa mfano wa mtumishi wa namna hii. Alijitolea kwa ajili ya Bwana, aliyatoa maisha yake kusaidia kueneza utawala wa Kristo. Mimi na wewe tunapaswa kuwa watumishi wa namna hii. Tujitoe kwa ajili ya Bwana. Tueneze utawala wa Bwana. Tuchunguze picha, maneno na message tunazotuma au kuongea hasa hasa katika simu zetu. Baadhi zinasaidia kueneza utawala wa shetani. Pia tuchunguze namna tunavyotumia rasilimali zetu. Matumizi mengine kama katika ulevi na uasherati yanasaidia kueneza utawala wa shetani.
Pia tutambue wajibu wetu katika kuwaangazia wenzetu. Tumeitwa ili wenzetu wapate unafuu kwa uwepo wetu. Tuepuke kuwa kero kwa wenzetu. Tusisifike kwa tabia za ukorofi na kuwatesa wenzetu.
Katika somo la injili, Yohane anatangazwa kukua katika hekima, na alikaa katika jangwa. Jangwa ilikuwa sehemu ya kujitenga na malimwengu ili mtu aweze kumtumikia Bwana. Yeye kama mnaziri wa Bwana alichagua kukaa jangwani.
Sisi tujiulize, jangwa letu ni lipi? Upo wakati ninaoamua kwenda jangwani ili niweze kukaa na Bwana? Na kutafakari makuu yake? Bila kutafuta sehemu ya jangwa na kutafakari, hakika ni vigumu kuweza kuwa mtumishi wa Bwana. Jangwa letu laweza kuwa sehemu kama kanisani, au jumuiya, au vyama vya kitume. Sehemu kama hizi hutufundisha na kutuwezesha kukutana na Bwana. Tusiache kukaa jangwani. Jangwa litatupatia nguvu ya kuwa watumishi wema wa Bwana. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni