Jumatano, Juni 23, 2021
Jumatano, Juni 23, 2021
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa
Mwa 15: 1-12, 17-18;
Zab 105: 1-4, 6-9;
Mt 7: 15-20
HUKUNA MTI MZURI UNAO ZAA MATUNDA MABAYA!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza, Abrahamu anaanza kuingia katika wasiwasi juu ya ahadi ya Mwenyezi Mungu juu yake kuhusu uzao. Mwenyezi Mungu anakuja kwake na kumwakikishia kwamba hakika atapata huo uzao. Tena Mwenyezi Mungu anaweka naye agano ambapo anaamuru wanyawa wapasuliwe vipande kama sadaka. Halafu Mwenyezi Mungu Mwenyewe anapita juu ya vile vipande vya sadaka na kuziteketeza kwa moto. Kwa kufanya hivi, Mwenyezi Mungu alifanya agano na Abrahamu-kwamba hakika atatekeleza agano hilo.
Kila aliyekubali kupita juu ya sadaka ya kuteketezwa alimaanisha kwamba yeye Mwenyewe ameamua kujifunga; na yule atakayekataa kutimiza sehemu yake, basi atateketea kama hiyo sadaka. Hii ndiyo maana ya sadaka hii, na maana ya Mungu kupita juu yake. Hakika Mungu hutimiza ahadi zake. Lakini sisi kama wanadamu dhaifu, inafikia mahali tunaona kana kwamba Mungu hatimizi ahadi zake na tunaishia hata kukata tamaa. Lakini Mwenyezi Mungu anatueleza leo kwamba hakika yeye hutimiza ahadi zake.
Somo hili litutie moyo na sisi pia kwani upo wakati unafika ambapo tunajisikia kukata tamaa kabisa, tunaishiwa nguvu kabisa, tunafikiria kwamba tumesahauliwa na Bwana. Lakini leo tunagundua kwamba Mwenyezi Mungu anatukumbuka wakati wowote. Basi tusiruhusu shida zetu zifunike tumaini tulilonalo kwa Mwenyezi Mungu. Wengi tunaruhusu shida kutufunika kiasi cha kukosa matumaini. Hatupaswi kufanya hivi.
Abrahamu japokuwa alikuwa na uchungu, imani yake ilikuwa kubwa kwa Mwenyezi Mungu. Sisi tusiruhusu imani yetu kwa Mwenyezi Mungu ishindwe na shida zetu.
Katika somo la injili, Bwana Yesu anasisitiza kwamba mti mwema huzaa matunda bora. Na siku zote mti mbaya hauwezi kutegemea uzae matunda bora. Hivyo maisha yanahitaji matayarisho. Utakatifu unahitaji matayarisho. Bila bidii, usitegemee tuweze kufanya chochote chema maishani. Uvivu utatuangusha tu. Hivyo kama tunataka kuwa na vitu bora, basi tuanze kwa kufanya bidii tangu leo. Tufanya mambo yetu kwa mpangilio. Tumkaribishe mwenyezi Mungu atawale kila kitu.
Tumsifu Yesu Kristo...
Maoni
Ingia utoe maoni