Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Juni 22, 2021

Jumanne, Juni 22, 2021,
Juma la 12 la Mwaka wa Kanisa

Mwa 13: 2, 5-18;
Zab 15: 2-5;
Mt 7: 6, 12-14

NJIA NYEMBAMBA!

Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza, tunakutana na Abrahamu akiendelea kubarikiwa na Bwana na anachokifanya anamjengea Mwenyezi Mungu Altare kwa ajili ya kuabudu na kutolea sadaka. Na kwa kufanya hivi, anayatakasa makao yake, anamkaribisha Bwana kukaa kati yake na kubariki ardhi atakayokaa.
Sisi tubariki makao yetu tunayokaa kila siku. Tujitahidi kuyabariki kwa kujenga altare ndani ya makao yetu, ikimaanisha tuhakikishe kuna uwepo wa Mungu katika familia na maeneo tunayokaa, ukiwa hata na nyumba yako umejenga au ardhi yako, omba padre akusaidie kubariki, simika uwepo wa Mungu kabla ya kujitegemea mwenyewe, usiende kuzindika na manyoya ya kuku au madawa kutoka kwa waganga.
PiaTunapojenga makanisa au grotto ni namna mojawapo ya kumkaribisha Bwana katika makao yetu kama alivyofanya Abrahamu. Hivyo, tusiache kushiriki katika matendo ya namna hii.
Katika somo la injili, Yesu anasisitiza kwamba tusiwapatie mbwa matakatifu au tusiwapatie lulu zetu nguruwe. Mbwa na nguruwe walikuwa wanyama najisi kwa dini ya kiyahudi. Mbwa alionekana kutokujua matakatifu, hivyo, akipewa matakatifu, atayachana chana tu. Nguruwe alisifika kwa kuchafua na kukanyagakanyaga kila kitu. Hata kitu cha thamani, nguruwe alikanyaga tu. Hakujua tofauti kati yao.
Yesu anasema wapo wanadamu wa namna hii, wasioweza kutunza matakatifu. Watu wa namna hii, wasipewe matakatifu, au wasiambiwe watunze matakatifu au hata kupewa cheo katika kanisa. Au kuwaambia waoshe hata mambo matakatifu. Wapo kati yetu ambao kati yetu wakipewa Rozari au Biblia, unakuta wametupatupa kila mahali, wamechana chana, imewekwa hadi kwenye meza ya chakula, imechafuliwa kabisa na michuzi. Au ukikuta wamekwenda kuhiji na kupewa vyombo vitakatifu, watashindwa kuvitunza. Watachafua kila kitu. Watu wa namna hii, wasio na heshima kwa matakatifu wasipewe madaraka yoyote au kupewa wajibu wa kutunza matakatifu; kwani watayachana chana na kuyakanyaga kama nguruwe na mwishowe watu watakwazika na kushindwa kumfikia Mungu.
Sisi tuzidishe imani ndugu zangu. Tutunze vile tunavyovaa, kama unavaa rozari, ivae vizuri, tunza, isiwe chafu, halafu, kama imekatika, unapaswa kuitengeneza. Isiwe kama inayovaliwaga na nguruwe. Hili ni la muhimu sana ndugu zangu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni