Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Juni 11, 2021

Ijumaa, Juni 11, 2021,
Juma la 11 la Mwaka wa Kanisa

Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu

Kumb 7: 6-11;
Zab 103: 1-4;
1 Yn 4: 7-16;
Mt 11: 25-30


MOYO UNAO WAKA MAPENDO!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Leo ni sherehe ya Moyo Mt. wa Yesu. Huu ni moyo Mtakatifu sana. Ndani ya Moyo huu, yametoka mapendo makubwa sana kwa dunia. Mapendo ya Moyo huu yameiokoa dunia. Moyo huu ulilala juu ya msalaba na ukachomwa na kutoa damu na maji. Maji ni ishara ya utakaso na damu ni ishara ya upatanisho.
Moyo huu unaendelea kututakasa na kutupatanisha na Baba kila siku kwa njia ya sakramenti zote. Sakramenti zote za kanisa zinamwagika toka katika moyo huu. sisi tuushukuru Moyo huu. Tuzitumie vyema sakraementi zinazobubujika katika moyo huu. Sisi nasi tuombe kuwa na moyo wenye kufanana hivi. Mioyo ya namna hii itailetea dunia faraja na matumaini.
Katika somo la kwanza, Musa anawaeleza kwamba Israeli inauonja upendo wa Mwenyezi Mungu sio kwa sababu ya mastahili yake mwenyewe; bali ni upendo wa Mwenyezi Mungu aliyewachagua na kuwapa upendeleo. Wanapaswa kutoa shukrani kwa upendeleo huu kwa kuzishika amri za Mwenyezi Mungu. Leo kila mmoja wetu atambue kwamba somo hili linamhusu kila mmoja. Kila mmoja ajichunguze na kuona namna jinsi alivyobarikiwa. Kuna vipawa na tunu ambazo ziko kwangu lakini kwa mwingine haziko. Lazima kipo kitu kama hiki. Tunachopaswa kutafuta leo ni kuzichambua tunu za namna hii na kuzikuza. Wengi hatujiangalii na kuzitunza tunu zetu. Na hata baadhi yetu hatutambui hata vipawa tulivyokwishapewa tayari. Bado tunaangalia vya wenzetu na kuvionea wivu.
Mungu anakutaka leo utunze ile tunu aliyokujalia. Yaweza kuwa ni tunu ya utii, uaminifu, busara, uchapaji wa kazi. Kwa njia ya tunu aliyokujalia, hakika atakuinua. Huu ndio upendeleo alioujalia kwa kila mmoja.
Katika somo la Injili, Bwana Yesu anadhihirisha kwamba moyo wake ni moyo unaokaribisha. Unakaribisha wote wenye njaa na kiu na wote watapumzishwa. Tunachopaswa kujitia nira ya Yesu na kujifunza kwake. Nira ni kifaa kinachodhibiti wanyama wanaofanya kazi ili wasitende kilichotofauti. Sisi tunapaswa kujitia nira ya Yesu. Wengi wetu tumejitia nira za shetani. Hivyo, maisha yetu kila siku ni kufanya ya kishetani. Tuvue nira za shetani. Nira za shetani tulizovaa ni nira za ulevi, urafiki mbaya, ulafi, matumizi mabaya ya simu. Yote haya ni nira zinazotutesa. Tujitwike nira za Yesu.
Yesu anaendelea kusema mambo haya yamefichwa kwa wenye majivuno. Wanaofaidi kuona haya ni wale tu walio wapole na wanyenyekevu wa Moyo. Sisi ndugu zangu tujitwike moyo mnyenyekevu na mpole. Mwenye upole na unyenyekevu ipo amani, ipo furaha, upo utulivu anaoufurahia vyema kuliko wewe. Hivyo, usiache kujitwika nyenzo hizi ndugu yangu. Hizi ndizo tunu za Moyo Mtakatifu wa Yesu. Hizi ndizo tunu zitakazotuokoa.

Maoni


Ingia utoe maoni